HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 24, 2021

MKUTANO WA KIMATAIFA WA ELIMU BORA WATOKA NA MAADHIMIO KAMBAMBE KUBORESHA ELIMU

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Gerald Mweli akizungumza alipokuwa akifunga Mkutano wa Kimataifa wa Elimu Bora ulioandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) na kufanyika jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bw. John Kalage akizungumza kwenye mkutano huo.
Sehemu ya wajumbe katika mkutano huo wakifuatilia hotuba ya Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, Bw. Mweli alipokuwa akifunga mkutano huo.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Gerald Mweli akizungumza na baadhi ya wanahabari (hawapo pichani) katika hafla ya katika hafla ya kufunga Mkutano wa Kimataifa wa Elimu Bora ulioandaliwa na TEN/MET.
Mratibu wa Taifa TEN/MET, Bw. Ochola Wayoga akisoma maadhimio ya mkutano huo kabla ya kufungwa rasmi na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Bw. Gerald Mweli.


MKUTANO wa kimataifa wa elimu Bora ulioandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) uliomalizika jijini Dar es Salaam, umetoa maadhimio lukuki ambayo yana lengo la kuiboresha elimu nchi ili iendane na mabadiliko na changamoto za sasa.

Akisoma maadhimio hayo kwa wanahabari mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo, Mratibu wa Taifa TEN/MET, Bw. Ochola Wayoga amesema wadau hao wa elimu wamepata fursa ya kutathmini elimu inayotolewa na kupendekeza ndani ya miaka mitano na zaidi ijayo elimu hiyo iweje kwa kuzingatia maboresho zaidi.

Alisema miongoni mwa mapendekezo ni elimu inayotolewa kuwa ni elimu jumuishi isiyobagua mtu yeyote, na lazima kuwepo na mifumo anuai inayosapoti elimu, huku wakipendekeza uwepo wa mifumo ya kuandaa mitaala, mifumo ya majadiliano katika kuboresha elimu na mifumo ya ulipaji walimu na stahili zao. 

"...tumependekeza elimu yetu lazima ibadilike na iendane na teknolojia (Teknohama) ili iendane na mabadiliko ya kiteknolojia. Na kwa elimu ya Chuo Kikuu iboreshwe na iendane katika kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika sekta hiyo...elimu ya chuo kikuu mitaala ilenge kutatua matatizo yaliyopo nchini, mfano wanafunzi wa chuo inatakiwa watoke vyuoni wakiwa na ujuzi  na ubora wa kutosha kukabiliana na mazingira yoyote ya vikwazo eneo hilo." Alisema Bw. Wayoga akisoma mapendekezo ya mkutanohuo.

Aliongeza kuwa Serikali inakila sababu ya kutathmini uwekezaji uliopo katika elimu kwa sasa kama unakidhi viwango na kama sivyo, Serikali na wadau wa elimu waongeze uwekezaji wa elimu ili kuboresha zaidi. Serikali iwekeze vya kutosha kwenye eneo hili, sasa tunawekeza asilimia 17 ya bajeti kwenye elimu lakini kiasi hiki bado ni kidogo tuongeze tena.

Hata hivyo, wamependekeza namna bora ya kufanya maboresho katika mitaala ya elimu kuanzia eneo la elimu ya awali, elimu ya msingi, elimu ya Sekondari na hata ngazi ya vyuo vikuu. Alisema elimu katika maeneo hayo haina budi kuendana na mahitaji ya dunia ya sasa na kazi za miaka 20 na miaka 50 ijayo. 

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Gerald Mweli akizungumza  akifunga mkutano huo alisema Serikali imepokea na kuridhia mapendekezo hayo huku akiahidi kuyafanyia kazi kila hali inaporuhusu.

Alisema Serikali imekuwa ikifanya maboresho ya elimu mara kwa mara na itaangalia pia namna ya kuyafanyia kazi mapendekezo hayo. Aliwataka wadau hao kuendelea na mjadala wa maboresho ya elimu kwani lengo ni mafanikio katika sekta hiyo, jambo ambalo litafanikiwa zaidi kwa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wengine.

Mkutano huo wa kimataifa juu ya elimu bora uliofunguliwa na Rais mstaafu Awamu ya Nne, Mhe. Jakaya Kikwete ulishirikisha wadau mbalimbali wa elimu ikiwepo serikali, wanachama wa mtandao, Washirika wa Maendeleo pamoja na wadau wengine wa elimu nchini.

No comments:

Post a Comment

Pages