May 31, 2021

NMB yazindua jukwaa la kuwawezesha vijana

 

 

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu, Patrobas Katambi  (wapili kulia), Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe (wa tatu kulia) na Afisa Mkuu wa wateja binafsi na Biashara Benki ya NMB, Filbert Mponzi (wa tatu kushoto), wakizindua kwa pamoja Jukwaa la Vijana ‘Go na NMB’ lenye lengo la kutoa elimu ya kifedha pamoja na fursa za mikopo kwa vijana. Uzinduzi huo ulifanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. (Na Mpiga Picha Wetu).


Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu, Patrobas Katambi  (watatu kulia), Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe (wapili kulia) na Afisa Mkuu wa wateja binafsi na Biashara Benki ya NMB, Filbert Mponzi (wa tatu kushoto), wakifurahia baada ya uzinduzi wa Jukwaa la Vijana ‘Go na NMB’.


 Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu, Patrobas Katambi  (watatu kulia), akipeana mkono na Afisa Mkuu wa wateja binafsi na Biashara Benki ya NMB, Filbert Mponzi, mara baada uzinduzi wa Jukwaa la Vijana ‘Go na NMB’.


Na Mwandishi Wetu
 
Benki ya NMB imeanzisha utaratibu wa kipekee wa kuwasaidia vijana nchini kupitia jukwaa la huduma suluhishi za kibenki utakaowawezesha kifedha na kuwakwamua kiuchumi.
 
Serikali imeukubali na kuunga mkono mpango huo wa huduma maalumu za kibenki kwa ajili ya vijana ambao kibiashara unaitwa ‘Go na NMB’ kwa sababu unaendana na sera zake za kuwashirikisha katika ujenzi na maendeleo ya taifa.
 
Katika hotuba yake ya kulizindua rasmi jukwaa hilo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira, Patrobas Katambi, alisema kuanzishwa kwake kumekuja wakati muafaka na ni uwekezaji stahiki.
 
Hii ni kutokana na umuhimu na unyeti wa kada ya vijana kwenye shughuli za uzalishaji mali kwani wao ni raslimali watu ya msingi kiuchumi na katika maendeleo ya nchi kwa ujumla. Kwa mantiki hiyo, naibu waziri huyo alifafanua, lazima vijana wawe na ufahamu mkubwa wa maswala ya pesa, wahusishwe kifedha, wasaidiwe kibiashara na kuwezeshwa kiuchumi.
 
“Jukwa la ‘Go na NMB’ ambalo ninalizindua rasmi leo linayazingatia hayo yote na ndiyo maana serikali inaliunga mkono kwani mikakati bunifu kama hii inatusaidia sana kuzikabili changamoto mbalimbali za vijana,” Katambi alisema.
 
Pia kiongozi huyo alisema kuwa sifa moja kubwa ya jukwaa hilo ni kutobagua vijana watakaonufaika nalo kwani lipo kwa ajili ya vijana wote wa Kitanzania. Wawe ni wakulima, walioajiriwa ua kujiajiri na hata wanafunzi wa vyuo vikuu na vya kawaida, wote watasaidiwa na kuhudumiwa, alisisitiza.
 
Benki ya NMB imesema jukwaa la ‘Go na NMB' ni maalumu kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya kibenki ya vijana lililoongezwa thamani kuwavutia ambalo litakuwa msingi wa kuwajenga na kuwapa uwezo wa kujitegemea kwa kuwapatia suluhishi za kifedha huku likitanguliza mbele maslahi yao pamoja na ndoto walizonazo.
 
Moja ya malengo ya NMB katika hili ni kuwahudumia vijana kisasa zaidi na ni mpango mkakati wake kupanua wigo wa wateja kwa kujenga mazingira bora ya huduma za kibenki kwa vijana ili wao na benki hiyo waweze kuchangia kikamilifu ukuaji wa uchumi wa taifa.
 
Jukwaa la ‘Go na NMB’ ambalo ni kwa ajili ya nchi nzima ni soko la rejareja kwa vijana litakalokuwa nembo maalumu ya huduma za kidijitali za NMB. Mkazo wa jukwa hilo la kwanza sokoni utaelekezwa kwa vijana wanaojishughulisha kwenye shughuli rasmi na zisizo rasmi hususani wanaojishughulisha na  kilimo, biashara ndogo ndogo na za kati pamonja na wanafunzi wa ngazi zote mpaka wa vyuo vikuu.
 
Akizungumza kwenye tamasha la uzinduzi wa ‘Go na NMB’ jijini Dar es Salaam, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Bw Filbert Mponzi, alisema kila kijana ana haki ya kupata huduma salama inayofikika kwa urahisi na yenye tija.
 
Ni kwa kuzingaitia hilo, na wajibu wake wa kuwasaidia ili wakue kama Watanzania wenye mchango kwenye uchumi na maendeleo ya nchi yao, ndiyo maana ‘GO na NMB’ imeanzishwa.
 
“Dhamira yetu ni kutanua wigo wa huduma zetu ili tuwafikie vijana wote. Hii itawawezesha vijana wengi zaidi kufikiwa na huduma za kifedha huku ikiwasaidia kujenga utamaduni wa kuwa na nidhamu ya fedha wanapoandaa maisha yao ya baadae hatua ambayo pia itakachangamsha uchumi wa nchi,” Mponzi alisema.
 
“Tunafanya haya yote tukiwa sambamba na malengo ya maendeleo ya Serikali yakiwemo ya utoaji wa huduma salama na bora za kifedha kwa jamii nzima,” alisisitiza na kuongeza:
 
“Takwimu mbalimbali zinaonyesha kuwa Tanzania ina vijana takribani asilimia 64 hivyo kufanya kundi hili kuwa sehemu muhimu ya ukuaji wa uchumi. Benki ya NMB imejipanga kuwafikia wote, kuanzia wanafunzi mpaka vijana wenye shughuli za uzalishaji kwenye sekta zote za uchumi.”
 
Awali, meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard, alisema faida na huduma wezeshi za kifedha za jukwaa la ‘Go na NMB’ ni nyingi na zenye tija kimaendeleo binafsi na taifa kwa ujumla.
 
Huduma hizo ni pamoja na kujiunga kidijitali, kupata nafasi ya kushiriki promosheni na kujishindia zawadi zitakazokuwa zinatolewa kupitia vituo vya mauzo vya NMB pamoja na kupata mikopo nafuu ya bodaboda na Pikipiki za miguu mitatu.
 
Nyingine ni bima ya bure ya simu za mkononi, mafunzo ya uelewa wa masuala ya kifedha na kupata fursa za kuhudhuria matukio mbalimbali kama makongamano ya wanafunzi vyuoni, fursa za mafunzo kwa wanafunzi na kupata huduma ya mtandao ya bure kwenye baadhi ya vyuo vikuu

No comments:

Post a Comment

Pages