HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 18, 2021

TANZANIA KUENDELEA KUONGZA KWA UZALISHAJI WA MPUNGA

.Mhandisi wa kilimo kutoka Wizara ya Kilimo Idara ya Mafunzo,Huduma za ugani na Utafiti Mhandisi Maregesi Geofrey akifungua Mkutano huo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Prof. SIza Tumbo.

Bi. Ridda Dally afisa miradi ya Kilimo kutoka Shirika la maendeleo la Japan (JICA) akitoa salamu za wadau wa zao la mpunga wakati wa ufunguzi wa mkutano huo.


Na Calvin Gwabara, Dar es Salaam


SERIKALI kwa kushirikiana na wadau wa zao la Mpunga nchini wameazimia kuimarisha utoshelevu wa chakula katika ukanda wa Afrika mashariki, Jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa jangwa la sahara (SADIC) na kuwa kinara wa soko la mchele katika jumuiya za kikanda kupitia mkakati wa taifa wa pili wa maendeleo ya Mpunga.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa wizara ya kilimo Prof. Siza Tumbo kwa niaba yake na Mhandisi wa Kilimo wizara ya Kilimo katika Idara ya Mafunzo huduma za ugani na Utafiti Mhandisi Maregesi Geofrey wakati akifungua Mkutano wa Kikanda  kuhusu mnyororo wa thamani wa zao hilo unaofanyika jijini Dar es salaam.

“Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na wadau wa zao la mpunga nchini tumejipanga kuhakikisha tunaongeza eneo la uzalishaji wa mpunga kutoka hekta milioni 1.1 za mwaka 2018 hadi hekta milioni 2.2 ifikapo mwaka 2030 na hivyo kuongeza uzalishaji kutoka tani 2.2 kwa hekta za sasa hadi kufikia tani 4.4 ifikapo mwaka 2030”Alisisitiza Mhandisi Maregesi.

Ameongeza kuwa mambo mengine ambayo yatatekelezwa ni kuimarisha mifumo ya masoko na biashara,kuongeza upatikanaji wa mbolea na usambazaji,kuimarisha kilimo cha umwagiliaji na kuhamasisha teknolojia zake sambamba na kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno kutoka asilimia 30 hadi 10 ifikapo 2030.

Aidha ameeleza kuwa zao la mpunga ni mojawapo wa zao muhimu la chakula linalozalishwa takribani mikoa yote nchini katika wilaya zaidi ya 26 ambazo kwa utafiti wa mwaka 2018 inazalisha tani milioni 2,219,628.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufuangua Mkutano huo, Mtafiti kiongozi na mkuu wa mradi huo kwa upande wa Tanzania Prof. Aida Isinika amewataka wadau wote kwenye mnyororo wa thamani wa zao la mpunga nchini  kujipanga ili kuhakikisha Tanzania inajitosheleza kwa zao hilo na kuendelea kuwa kinara wa uzalishaji wa Mpunga kwa nchi za Afrika mashariki.

 “Sote Tunajua kuwa Tanzania tunaongoza kwenye uzalishaji wa zao la Mpunga kwenye ukanda huu wa Afrika ya mashariki lakini lazima tutambue kuwa kuna nchi mbalimbali sasa zinakuja kwa kasi katika kuongeza tija hivyo ni lazima wadau wote tujipange ili nchi yetu izidi kuwa kinara na kushika soko la dunia” Alisisitiza Prof. Isinika.

Prof. Isinika amesema wazalishaji wakubwa wa Mpunga duniani uwezo wao kwenye tija umefikia mwisho na sasa wanaangalia bara la afrika kwakuwa bado lina fursa kubwa za uzalishaji na tija hivyo Tanzania lazima ijipange zaidi katika kutumia fursa nyingi zilizopo kuzalisha na kuuza nje ya nchi badala ya kutegemea kuingiza kutoka nje ya nchi.

Mkuu huyo wa mradi amewashukuru wadau wote kwenye mnyororo wa thamni waliokubali kushiriki mkutano huo muhimu ambao utaangalia maeneo yote muhimu hasa na kuja na maazimio ya njia bora ambazo zitasaidia kufikia malengo hayo ya taifa kwa pamoja .

Akitoa salamu kwa niaba ya wadau wengine wa mkutano huo kwenye mnyororo wa thamani afisa miradi ya kilimo  wa shirika la maendeleo la Japan (JICA) Bi. Ridda Dally amesema kwa miaka mingi wamekuwa wakishirikiana na wadau wengine na serikali katika kusaidia ukuzaji wa zao la mpunga nchini na wataendelea kushiriki ili kufikia malengo.

Amesema zao la mpunga ni moja ya mazao yanayochangia katika maendeleo ya wananchi na taifa ndio maana JICA waliamua kufadhili kikosi kazi kilichokuwa kikiandaa mpango mkakati wa kwanza na wa pili ambao lengo lake lilikuwa ni kuongeza uzalishaji wa zao hilo hivyo mkutano huo utasaidia kuja na mikakati bora itakayowezesha kufikia mpango huo wa serikali.

Mkutano huo wa siku tatu unahusisha wadau kwenye mnyororo mzima wa thamani wa zao hilo hapa nchini ambapo kwa siku ya kwanza wanajadili mipango ya Tanzania na siku ya pili nay a tatu mkutano utajumuisha wadau kutoka nchi zote duniani ambapo zaidi ya wadau 500 watashiriki kwa njia ya mtandao.

No comments:

Post a Comment

Pages