May 07, 2021

WAKANDARASI ACHENI UBINAFSI UNGANENI TUWAPE KAZI- WAITARA


 

 Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Iddy Kimanta (kulia), akijadiliana jambo na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mwita Waitara walipokutanamjini Arusha. 

 


Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Mwita Waitara amewataka wakandarasi nchini kuungana na kuacha chuki, ubinafsi na fitna ili wanufaike na miradi mingi ya ujenzi inayotekelezwa na Serikali.

Amesema hayo leo jijini Arusha wakati akifungua mkutano wa pili wa mashauriano wa wadau wa sekta ya ujenzi kwa mwaka 2021 ulioandaliwa na Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB), na kusisitiza nia ya serikali kufanya kazi na wakandarasi walioungana, waadilifu na wenye gharama nafuu.

“ Miradi mingi mikubwa ya Serikali inafanywa na wakandarasi wageni kutokana na wakandarasi wazawa kushindwa kuungana na kuitekeleza kwa ubora na kwa muda unaotakiwa”, amesema.

Serikali imejipanga kutoa kipaumbele kwa wakandarasi wazawa watakaojiunga ili kuwajengea uwezo wa kimtaji na kuwawezesha kumudu  kujenga miradi mikubwa na hivyo kubakisha fedha nyingi za miradi hiyo hapa nchini.

“Mkipewa miradi wekeni gharama nafuu na ikamilisheni kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa ili kujenga imani kwa Serikali na wananchi kuwa wakandarasi wa ndani wanaweza”, amesisitiza Waitara.

Amewataka wakandarasi kupambana na rushwa katika miradi na pale wanapoungana kuwa na nidhamu ya ushirika ili kuwezesha miradi wanayopata kukamilika kwa wakati, ubora  na kwa gharama nafuu.

Naibu Waziri Waitara amewataka wadau wa ujenzi kufanya tathmini kuhusu gharama za ujenzi nchini ili kuja na bei nafuu itakayowezesha miradi mingi ya Serikali  kufanywa na wakandarasi wazawa na hivyo kuongeza fursa za ajira na kukuza uchumi.

Naye Mwenyekiti wa CRB,  Mha. Consolatha Ngimbwa ameiomba Serikali kutumia wakandarasi waliosajiliwa ili kuwezesha ujenzi nchini kuwa wa viwango vya juu na kutoa fursa za ajira kwa watu wengi.

“ Hali ya wakandarasi nchini ni mbaya kutokana na matumizi ya force account kwenye miradi mingi ya serikali na hivyo kuwafanya wakandarasi wengi kukosa kazi amesema Mha. Ngimbwa.

Amesema CRB imewafundisha wakandarasi wake namna bora ya kutayarisha zabuni na kusimamia miradi ya ujenzi ili ikamilike kwa wakati.

“Wakandarasi tuko tayari tunaomba tupewe tujenge mji wa serikali na tulipwe kwa wakati”, amesisitiza Mha. Ngimbwa.

Naye msajili wa wakandarasi nchini Bw, Reuben Nkori ameiomba serikali iweke vituo vya kukodisha mitambo ili kuwawezesha wakandarasi kupata vifaa kwa urahisi, ipambane na rushwa katika usimamizi wa miradi na kuwalipa wakandarasi kwa wakati ili kuwezesha miradi kuwa nafuu.

Mkutano huo wa siku mbili wa mashauriano unaoongozwa na kaulimbiu “ juhudi za makusudi za wadau kuwezesha ukuaji wa wakandarasi wa ndani”, pamoja na mambo mengine utajadili na kutoka na ufumbuzi wa namna bora ya kuwezesha wakandarasi wazawa na sekta ya ujenzi nchini kukua.

Takriban wakandarasi 11,600 wamesajiliwa nchini na kati yao asilimia 3.5 ni wakutoka nje na 96.5ni wazawa ambao wako tayari kufanya kazi kwa ubora unaozingatia thamani ya fedha.


No comments:

Post a Comment

Pages