May 07, 2021

Wazazi, wadau, Serikali watakiwa kuwekeza kwenye riadha ya vijana

Muasisi wa Arusha Youth Athletic Championship, Juliana Mwamsuva akielezea kwanini ameamua kujikita katika eneo hilo la kuibua vipaji vya vijana wanaopenda riadha nchini. 

 

NA SULEIMAN MSUYA, ARUSHA


WAZAZI, wadau na Serikali wametakiwa kuwekeza kwenye mchezo wa riadha kuanzia ngazi ya chini kwa kuwa ni chanzo cha ajira.

Hayo yamesemwa na Muasisi wa Mashindano ya Arusha Youth Athletic Championship, Juliana Mwamsuva wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii.

Mwamsuva amesema ili mchezo wa riadha uweze kukuwa ni lazima kuwepo na uwekezaji kuanzia ngazi ya chini ili kupata wanariadha wengi.

Amesema wakiambiaji wenye rikodi nzuri za kimataifa mwanzo wao umeanzia ngazi ya chini hivyo familia, wadau na Serikali inapaswa kuwekeza katika eneo hilo.

Muasisi huyo amesema wazazi na familia kwa ujumla wanapaswa kubadilika kuhakikisha wanawashawishi watoto kushiriki riadha.

"Mchezo wa riadha unalipa iwapo maandalizi yataanza utotoni kwa kila mzazi na familia kuwa chachu," amesema.

Mwamsuva amesema iwapo mwamko utakuwa mkubwa wadau wengi watajitokeza kufadhili riadha nchini.

Aidha, amesema mafanikio ya Arusha Youth Athletic Championship yanawasukuma kuandaa mashindao ya vijana ya Kimataifa.

Amesema baada ya mashindano ya mwaka jana uhitaji wa washiriki kutoka mikoa mingi ni mkubwa hivyo watahakikisha hitaji hilo linapatiwa ufumbuzi kwa kuandaa mashindao yenye sura ya nchi.

No comments:

Post a Comment

Pages