June 11, 2021

Magonjwa yasiyoambukiza huchangia theluthi 2 ya vifo



 Mkurugenzi wa Afya na Lishe ya Jamii kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Ray Masumo akisoma hotuba yake wakati wa kufunguwa semina kwa waandishi wa habari iliyokuwa na lengo la kuwajengea uwezo wanahabari kuhusiana na ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha ili kuepuka jamii kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza leo Juni 10,2021 katika ukimbi wa mikutano wa tasisi hiyo jijini Dar es Salaam.

 

Na Suleiman Msuya


IMEBAINISHWA kuwa magonjwa  yasiyoambukiza kama kisukari, saratani, moyo na mfumo wa njia ya hewa husababisha theluthi mbili ya vifo duniani.


Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Jamii na Lishe wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dk.Ray Masumo wakati akifungua semina ya siku moja kwa waandishi wa habari kuhusu ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha katika kukabiliana na magonjwa sugu yasiyoambukiza iliyofanyika jijini Dar es Salaam.


Dk. Masumo amesema theluthi mbili hiyo ya magonjwa hayo yamebainishwa na Shirika la Afya Dunia (WHO) na kwamba asilimia 80 ya vifo hivyo vinavyotokea katika nchi zenye kipato cha chini na kati.


“Kulingana na uchunguzi wa hivi karibuni juu ya tatizo la viashiria  hatarishi vya magonjwa haya nchini Tanzania, kasi ya kuenea kwa ugonjwa wa kisukari na magonjwa ya moyo ni kubwa, na kuenea kwa shinikizo damu inakadiriwa kuwa ni zaidi ya asilimia 26,” amesema.


Amesema kutokana na kasi hiyo TFNC imelazimika kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari ikiamini kuwa ni wadau muhimu katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora katika kukabiliana na magonjwa hususani magonjwa yasiyo ya kuambukiza.


“Leo tumekusanyika hapa kwa lengo la kuwajengea uwezo kuhusu ulaji unaofaa na mitindo bora ya maisha ili kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.


Magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni magonjwa ambayo husababishwa na ulaji usiofaa na mitindo bora ya maisha. Magonjwa haya hayawezi kuambukiza mtu mwingine. 


Viashiria hatarishi vya magonjwa yasiyoambukiza ni pamoja na ulaji usiofaa hasa wa vyakula vyenye chumvi nyingi, mafuta mengi na sukari nyingi, uzito uliozidi na unene uliokithiri, kutofanya mazoezi na matumizi ya sigara na bidhaa za tumbaku,” amesema. 


Dk. Masumo ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TFNC amesema tafiti za kisayansi zinathibitisha kuwa sababu za magonjwa haya, zinaweza kugawanyika katika sehemu mbili; sababu zinazoweza kurebishika na zisizoweza kurebishika.


Ametaja sababu ambazo zinaweza kuzuilika ni ulaji usiofaa, kutoushughulisha mwili au kutokufanya mazoezi, matumizi ya tumbaku na matumizi mabaya ya pombe.


“Kwa upande mwingine sababu zisizoweza kuzuilika  hujumuisha uchafuzi wa hali ya hewa ndani na nje ambao husababisha magonjwa ya mfumo wa upumuaji na magonjwa ya moyo. Hata hivyo magonjwa haya yanaweza kuzuiliwa, kwa vile yanatokea mapema katika kipindi cha maisha kama matokeo ya mienendo ya maisha,” amesema. 


Amesema magonjwa hayo yanaweza kuzuilika na kudhibitiwa kwa kufuata taratibu sahihi zinazohusiana na ulaji unaofaa na mitindi bora ya maisha ikiwemo kuepukana na matumizi ya tumbaku, ulaji usiofaa, kutofanya mazoezi na  kazi za kushughulisha mwili na  matumizi ya pombe yaliyopitiliza.


Masumo amesema ongezeko la magonjwa haya huleta athari kwa maendeleo ya Taifa na jamii ikiwemo kuleta athari ya kutofikia malengo ya maendeleo endelevu kufikia mwaka 2030, ambayo yanajumuisha kupunguza vifo vya kabla ya wakati vitokanavyo na magonjwa haya kwa theluthi moja.


“Kwa kutambua athari zitokanazo na ulaji usiofaa na magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza kwa taifa na jamii Tanzania imechukua jitihada mbalimbali za kukabiliana na tatizo hilo ambazo ni pamoja na;


Kuhamasisha umma wa Watanzania kupitia  vyombo vya habari, na njia mbalimbali za utoaji elimu kwa umma, kushirikiana na wadau wa maendeleo kufanya tafiti mbalimbali zinazolenga kutambua ukubwa wa tatizo la magonywa yasiyo ya kuambukiza na namna bora ya kuweza kukabiliana nalo. Kuandaa miongozo mbalimbali ya ulaji unaofaa na mitindo bora ya maisha,” ameeleza.


Aidha, amesema TFNC kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikifanya upimaji wa viashiria hatari vya magonjwa sugu na kutoa ushauri nasaha jinsi ya kuzingatia taratibu sahihi za ulaji unaofaa na mitindo bora ya maisha ili kujikinga na magonjwa hayo.


Amesema pia taasisi imekuwa ikihamasisa umma kuhusu upimaji wa hiari wa viashiria hatarishi vya magonjwa sugu.


“Ninyi ni miongoni mwa wadau wakuu wa mawasiliano yanayolenga kubadili mitazamo na tabia za jamii kuhusu masuala

 ya lishe na afya. Nina uhakika kwamba baada ya semina hii mtakuwa na uelewa mpana zaidi kuhusu ulaji unaofaa na mitindo bora ya maisha katika kukabiliana na magonjwa sugu yasiyoambukiza,” amesema.


Kwa upande wake Ofisa Lishe Mtafiti Mwandamizi Maria Ngilisho amesema ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi hasa yenye asili ya wanyama huchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la lehema mwilini.


Amesema kiasi kikubwa cha lehemu mwilini husababisha mkusanyiko  wa mafuta katika mishipa ya damu hivyo kuzuia damu kupita kwa urahisi.
“Vyakula vyenye lehemu nyingi ni nyama,  mayai, jibini na maziwa yasiyotolewa mafuta, maini, moyo, firigisi na figo”. amesema.


Mtafiti huyo amesema unywaji maji safi, salama na ya kutosha ni sehemu ya mlo kwani yana umuhimu kiafya hivyo inashauriwa kunywa maji safi na salama angalau lita moja na nusu kwa siku.

Ofisa Lishe Mtafiti Mwandamizi Julieth Shine amesema kuwa ulaji unaoshauriwa kwa mtu mwenye shinikizo kubwa la damu ni pamoja na kuepuka vyakula vyenye chumvi nyingi na vile vilivyosindikwa kwa chumvi hivyo unatakiwa kutumia viungo mbalimbali  kuongeza ladha ya chakula kwa mfano tangawizi, ndimu, vitunguu saumu na mdalasini.

No comments:

Post a Comment

Pages