June 11, 2021

Serikali yakihimiza UDSM, taasisi za elimu kufanya tafiti za Elimu ya Watu Wazima


Afisa Elimu ya Watu Wazima Mkoa wa Mwanza, Josephat Shaija akitoa majumuisho ya Kongamano la Kuadhimisha Miaka 50 ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania.

Wadau.
Baadhi ya washiriki wa Kongamano la Kimataifa la Kuadhimisha Miaka 50 ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye, akitoa hotuba yake wakati wa kufunga Kongamano la Kimataifa la Kuadhimisha Miaka 50 ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania.



Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga, akifunga Kongamano la Kimataifa la Kuadhimisha Miaka 50 ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye (kushoto), akimkabidhi tuzo Naibu Waziri  wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga ya kutambua mchango wa wizara hiyo katika kufanikisha Kongamano la Kimataifa la Kuadhimisha Miaka 50 ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania. 

Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga, akimkabidhi tuzo Prof. Victor Mlekwa (katikati) kwa kutambua mchango wake katika kufanikisha kongamano hilo.
Mshiriki kutoka Nigeria, Dk. Danlanin Hayyo akipokea cheti kutoka kwa mgeni rasmi.
Dk. Titilayo Adeoye Ajadi akipokea cheti kutoka kwa Naibu Waziri.
Mshiriki kutoka Ujerumani akionesha cheti baada ya kukadhiwa na mgeni rasmi.
 


Hussein Ndubikile, Dar es Salaam


Serikali imekihimiza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na  Taasisi nyingine za elimu kufanya tafiti zitakazosaidia kutoa machapisho na majarida yatakayoisaidia kuleta hamasa na msukumo wa jamii kushiriki katika elimu ya watu wazima ili kusaidia kuendelea kupunguza kundi la watu wasiojua kusoma, kuhesabu na kuandika pamoja  na kuchochea maendeleo endelevu.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga katika Kilele cha Kongamano la Kimataifa la Kuadhimisha Miaka 50 ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania lililoandaliwa na chuo hicho kupitia Shule Kuu ya Elimu.

Amesema chuo hicho kwa kushirikiana na taasisi nyingine za elimu kina wajibu wa kufanya tafiti zitakazosaidia kutatua changamoto zinazoikabili elimu ya watu wazima kwa kutoa machapisho na majarida yatakayosaidia jamiii kuondokana na ujinga.

" Nakihimza UDSM na taasisi za elimu mshirikiane katika utafiti wa elimu hii kisha mchapishe machapisho na majarida ya kutoa hamasa na kuhimiza jamii ishiriki katika madarasa ya MEMKWA," amesema Naibu Waziri Kipanga.

Amebainisha kuwa Serikali iko tayari kushirikiana na chuo hicho kwa kuhakik,isha elimu hiyo inawafikia watu wote wenye mahitaji nayo hivyo alikiomba UDSM kuendelea kushirikiana na wadau wa elimu kutatua changamoto zinazoikabili elimu hiyo.

Ameiomba Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU) kukipatia idhini chuo hicho kuanza kutoa Shahada ya Uzamili ya Ellimu ya Watu Wazima na kukipongeza kwa kuandaa kongamano hilo la siku tatu lililojadili mada kuhusu elimu hiyo.

Kwa upande wake Amidi Mkuu wa Shule hiyo  Daktari Eugenia Kafanabo amesema kongamano hilo lilijadili mada mbalimbali ikiwemo mchango wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere katika kuipigania na kuhamasisha jamii kushiriki katika kupata elimu hiyo pamoja na kuweka msisitizo wa kufufua madarasa ya elimu ya watu wazima..

Naye Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa William Anangisye amesema chuo hicho kitaekeleza agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa la kufanya tafiti kuhusiana na changamoto na majibu yake kwani katika mwaka wa fedha 2021/22 kimetenga Sh Bilioni 2 kwa ajili ya tafiti.

Profesa Anangisye amesema kongamano hilo lmeleta fursa ya wadau wa elimu hiyo kuwaleta pamoja ambapo walibalishana uwezo na mawazo kwa kujadili mada mbalimbali za kuendelea kuimarisha utoaji wa elimu hiyo nchini.

Afisa Elimu ya Watu Wazima kutoka Mkoa wa Mwanza Josephat Sheja amesema kongamano hilo limetoa maazimio mbalimbali ikiwemo Maafisa elimu mikoa na wilaya kuboresha madarasa ya MEMKWA kwa kuboresha programu, Serikali kuangalia uwezekano wa kuifanya elimuhiyo kuwa na idara inayojitegemea pamoja na wahitimu wenye vyeti,  shahada kutambuliwa katika muundo wa utumishi wa umma.


No comments:

Post a Comment

Pages