June 29, 2021

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wazinduliwa

 


Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, akizindua Kitabu cha Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano jijini Dodoma. Kushoto kwa Waziri Mkuu  ni Spika wa Bunge la Tanzania,  Job Ndugai. Kuanzia kulia kwa Waziri Mkuu ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango  Mhandisi Hamad Yusuff Masauni, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete na Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Bajeti Mhe. Daniel Sillo.

 

Na Jasmine Shamwepu, Dodoma


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022–2025/2026 utakaogharimu shilingi trilioni 114.8 huku akiwaonya watu wanaokwepa kodi.

 

“Serikali itahakikisha malengo ya Mpango huu yanafikiwa na kamwe hatutafumbia macho tabia ya watu kukwepa kulipa kodi wazembe kazini, ufujaji wa fedha na rushwa,lakini pia  tutaendelea kuenzi bunifu na kupokea mawazo mbadala yenye lengo la kuboresha utekelezaji wa Mpango huu.”alisisitiza Waziri Mkuu Majaliwa

 

Aidha alisema,Mpango huo umejikita katika kujenga  uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu huku ukijikita katika kuchochea uchumi shindani na shirikishi, kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma, kukuza uwekezaji na biashara, kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu.

 

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo jana jijini hapa wakati akizindua Mpango huo huku akisema Sekta binafsi inatarajiwa kuchangia kiasi cha shilingi  trilioni 40.6 na sekta ya umma shilingi trilioni 74.2.

 

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa ,fedha hizo zinajumuisha mikopo na misaada ya wabia wa maendeleo huku akisema Serikali itahakikisha fedha hizo zitapatikana  kiwa ajili ya kufikia malengo yaliyowekwa katika utekelezaji wake.

 

Vile vile alisema,katika Mpango huo Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya kielelezo ukiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ,ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115, ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta (EACOP) na ununuzi wa meli na ujenzi wa bandari ya uvuvi (Mbegani).

 

Aidha alisema, Mpango huo ni mkakati mahsusi wa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Mwaka 2020 huku akiwaahidi wananchi kuwa mambo yote yaliyoahidiwa  wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2020, yanaenda kutekelezwa kupitia Mpango huo.

 

Pia alisema,Mpango huo umezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025,Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2020,Mpango Elekezi wa Muda Mrefu 2011/2012–2025/2026 na Matokeo ya Tathmini Huru ya utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/2017–2020/2021.

 

Alisema, mpango huo pia umezingia sera na mikakati mbalimbali ya kisekta, matokeo ya tafiti zilizofanywa na vyuo na taasisi mbalimbali nchini, Dira ya Afrika Mashariki 2050, Dira ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika 2050, Ajenda 2063 ya Maendeleo ya Afrika,Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030,na Makubaliano ya Paris chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi.

 

Aliiasa Wizara ya Fedha na Mipango kuendelea na  utaratibu wa kutoa elimu ya kutosha ili kumwezesha kila mmoja kushiriki kikamilifu katika utekelezaji.

 

Aidha alitumia fursa hiyo kuwaziagiza  Wizara, Taasisi za Umma, Idara Zinazojitegemea Wakala za Serikali, Sekta Binafsi na Wadau wote wa maendeleo kuhakikisha ofisi zao zina nakala ya Mpango huo kwa ajili ya kuutekeleza.

 

Awali ,Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba alisema Mpango huo ni mwendelezo wa jitihada za Serikali za kuimarisha upangaji mipango na kusimamia rasilimali za ndani ya nchi ikijumuisha rasilimali za madini, maliasili, gesi asilia, ardhi, fedha na rasilimali watu kwa lengo la  kuboresha hali ya maisha ya Watanzania wote.

 

“Ili kuhakikisha Mpango huu unatekelezwa kwa ufanisi na unafikia malengo yaliyopangwa, Wizara imeandaa mwongozo wa kitaifa wa ufuatiliaji na tathmini wa miradi na programu za maendeleo na mfumo wa kitaifa wa kusimamia miradi ya maendeleo.”alisema Tuhuba

Alisema,Mpango huo umejikita katika maeneo matano ikiwemo kuimarisha uwezo wa uzalishaji na utoaji huduma,kuongeza thamani ya mazao,kukuza uwekezaji hasa kwa vijana ili waweze kujiajiri pamoja na kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza maarifa na ujuzi .

 Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Nchini Tanzania, Christine Musisi alisema wananchi, Serikali, wadau wa maendeleo, sekta binafsi watautumia mpango huo kama nyenzo muhimu ya utekelezaji wa kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030.

 

 Pia ameihakikishia Serikali kwamba mashirika yote ya Umoja wa Mataifa yataunga mkono utekelezaji wa mpango huo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.


No comments:

Post a Comment

Pages