June 29, 2021

SERIKALI YAWAPONGEZA SATF KWA KUWAHUDUMIA WATOTO 423 WENYE MAZINGIRA MAGUMU



 Katikati ni Mwaklishi wa Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Jeremy Divis, akikagua bustani ya mboga katika kijiji cha Litapwasi Halmashauri ya Wilaya ya Songea ambako  kaya masikini zimepewa msaada kupitia mradi wa tuwalinde watoto (PEPFAR) unaofadhiliwa na Ubalozi wa Marekani.

 

Serikali mkoani Ruvuma imelipongeza Shirika lisilo la kiserikali la  Social Action Trust Fund (SATF) kwa kuwahudumia watoto 423 wanasoma shule za msingi na sekondari kutoka kaya masikini 120 mkoani Ruvuma.

Pongezi hizo zimetolewa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Pololet Mgema wakati anazungumza na viongozi waandamizi wa SATF katika ziara yao ya kuzikagua kaya hizo  wilayani Songea.

Mgema amelishukuru shirika la SATF kwa kuhudumia Halmashauri tatu zilizopo mkoani Ruvuma,hata hivyo amemuomba Mwakilishi wa Balozi wa Marekani kuona uwekezekano wa kuhudumia Halmashauri zote nane kwa kuwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu wapo Mkoa mzima.

Naye Mwakilishi wa Balozi wa Marekani Jeremy Divis akizungumza baada ya kutembelea kaya masikini na kukagua miradi ya bustani kupitia mradi wa tuwalinde unaofadhiliwa na Balozi wa Marekani amefurahishwa na bustani za mboga zilizolimwa na kaya masikini.

Hata hivyo ameahidi kulifanyia kazi pendezo la Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,kuhakikisha kuwa mradi huo unatekelezwa katika Halashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma ili mradi uwe na tija kwa jamii ya wak zilizolimwa na kaya masikini

Afisa Mwandamizi wa SATF Sylvia Ruambo amesema Shirika hilo linahudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu tangu mwaka 1998 na kwamba mtoto anahudumia katika elimu kwa kuhakikisha anapatiwa vifaa vya shule.

“Licha ya kwamba mtoto anapewa vifaa vya shule,lakini SATF pia inampatia matibabu,msada wa kisaikolojia,ulinzi wa mtoto,pia kuna familia ambazo zinawezeshwa kiuchumi’’,alisema.

Kwa mujibu wa Afisa Mwandamizi huyo,hadi sasa SATF inafanyakazi katika mikoa 16 na Halmashauri 32 Tanzania bara na kwamba makao makuu ya Shirika hilo yapo jijini Dar es salaam.

Hata hivyo amesema SATF inafanya kazi kwenye mikoa na Halmashauri kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yamesajiriwa katika maeneo husika ambapo mashirika hayo yanasaidia kuibua watoto wenye sifa ya kusaidiwa na SATF.

Amesema mtoto anayesaidiwa na SATF anapewa vifaa vyote vya shule kuanzia shule ya msingi,sekondari hadi chuo kikuu na kwamba mtoto ambaye atashindwa kwenda hadi chuo kikuu,SATF inamsaidia kwenda katika vyuo vya ufundi ili kupata ujuzi ambao utamsaidia kujitegemea.

Amesema mtoto anapohitimu elimu ya ufundi SATF inamnunulia vifaa vyote vya  kufanyia kazi kulingana na fani aliyosomea ambapo amelitaja lengo la SATF ni kuhakikisha kijana aliyepata ujuzi anakuja kuwa mwanajamii mwenye tija kwa kujiajiri mwenyewe na kufanyakazi katika jamii husika.

Kuhusu afya Ruambo anasema SATF imekuwa inawapatia kadi za mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii iliyoboreshwa(ICHF)  ambapo anapewa mtoto na watu wengine watano kwenye familia yake na kwamba mtoto wa kike anapatiwa pia taulo za kike na nguo za ndani ambazo zitamsaidia kwa mwaka mzima.

Akizungumzia SATF katika Mkoa wa Ruvuma,Ruambo amesema  katika Mkoa wa Ruvuma,Shirika hilo linahudumia Halmashauri tatu ambazo ni Nyasa,Madaba na Halmashauri ya wilaya ya Songea na kwamba limeanza kuhudumia watoto 103 mwaka 2019 katika wilaya ya Nyasa .Hata hivyo amesema mwaka 2020 waliongezeka watoto wengine 80 hivyo kuhudumia watoto 183 katika Wilaya ya Nyasa.

Ruambo amesema mwaka 2021 SATF ilipata mradi kutoka mfuko wa Balozi wa Marekani ambao unaitwa tuwalinde watoto wetu kwa lengo la kuwasaidia watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu,walio katika hatari ya kutendewa ukatili na walipo kwenye hatari za virusi vya UKIMWI.

Amesema mradi huo katika Mkoa wa Ruvuma unatekelezwa katika Halmashauri tatu ambazo ni Madaba,Nyasa na Halmashauri ya Songea ambao umelenga kuhudumia watoto 240 ambao wanatoka kwenye kaya masikini 120.

Kupitia mradi huu watoto na walimu wao wamefundishwa haki na wajibu wa mlinzi wa mtoto,pia wanapatiwa vifaa vya elimu na bima ya afya hivyo  katika mkoa wa Ruvuma SATF inahudumia watoto 423 kuanzia ngazi ya shule ya msingi hadi sekondari.

SATF imezitembelea kaya masikini katika Halmashauri ya Songea kata za Peramiho,Litisha na Litapwasi ambapo kaya zilifundishwa namna ya kutengeneza bustani ili kupata mboga  za kuongeza lishe na kuwapatia kipato.

Naye Meneja wa Program wa SATF Nelson Rutabanzibwa akizungumza baada ya kukagua kaya hizo,amesema wameridhishwa na bustani zilizotengenezwa na kaya masikini ambapo hivi sasa wanakwenda kuwapatia mitaji ili waweze kufuga na kufanya biashara ndogo ndogo zitakazosaidia kuendesha maisha yao.

Rutabanzibwa amesema katika nchi nzima hadi sasa SATF imeshahudumia watoto karibu laki mbili na kwamba SATF inafanyakazi kwa kushirikiana na serikali ambapo mradi huu unatarajia kukamilika baada ya mwaka mmoja.

No comments:

Post a Comment

Pages