June 11, 2021

TFNC: Mtindo wa maisha chanzo magonjwa yasiyoambukiza



Ofisa Lishe Mtafiti Mwandamizi Julieth Shine, akitoa mada katika semina ya wanahabari kuhusu ulaji unaofaa na mitindo bora ya maisha katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.


Ofisa Lishe Mtafiti Maria Ngilisho, akitoa mada katika semina ya wanahabari kuhusu ulaji unaofaa na mitindo bora ya maisha katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.

 

Na Irene Mark


WATANZANIA wametakiwa kubadili mtindo wa maisha kwa kula makundi matano ya vyakula kwa wakati mmoja na kufanya mazoezi ili kujikinga na magonjwa sugu yasiyoaambikizwa.

Magonjwa sugu yasiyoambukiza ni Kisukari, saratani, shinikizo la damu na moyo.

Akizungumza wakati wa semina ya wanahabari kuhusu ulaji unaofaa na mitindo bora ya maisha katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza, iliyoandaliwa na Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Ofisa Lishe Mtafiti Mwandamizi, Adelina Munuo amesema hakuna njia sahihi ya kukabiliana na magonjwa hayo iwapo mtu atashindwa kuzingatia mlo wake.

Katika semina hiyo ya siku moja iliyofanyika Dar es Salaam leo Juni 10, 2021 Munuo aliwataka wanahabari kuwa chanzo cha madiliko na kuielimisha jamii umuhimu wa kuzingatia ulaji unaofaa ili kuepuka magonjwa yasiyoambukizwa ambayo ni mengi zaidi duniani.

“Kila siku jitahidi kula vyakula vyenye asili ya nafaka na mizizi, jamii ya kunde na nyama, mbogamboga, matunda, sukari na mboga zenye mafuta... vyote viliwe kwenye mlo mmoja kidogo kidogo na tufanye mazoezi,” amesema Munuo.

Ofisa Lishe Mtafiti Maria Ngilisho amesema ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi hasa yenye asili ya wanyama huchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la lehema mwilini.

“Kiasi kikubwa cha lehemu mwilini husababisha mkusanyiko  wa mafuta katika mishipa ya damu hivyo kuzuia damu kupita kwa urahisi. Vyakula vyenye lehemu nyingi ni nyama, mayai, jibini na maziwa yasiyotolewa mafuta.

Amesema unywaji maji safi, salama na ya kutosha ni sehemu ya mlo kwani yana umuhimu kiafya hivyo inashauriwa kunywa maji safi na salama angalau lita moja na nusu kwa siku.

Nae Ofisa Lishe Mtafiti Mwandamizi Julieth Shine amesema maendeleo ya kidunia yamesababisha watu wengi kuwa ulaji unaoshauriwa kwa mtu mwenye shinikizo kubwa la damu ni pamoja na kuepuka vyakula vyenye chumvi nyingi na vile vilivyosindikwa kwa chumvi hivyo unatakiwa kutumia viungo mbalimbali  kuongeza ladha ya chakula kwa mfano tangawizi na ndimu.

No comments:

Post a Comment

Pages