June 03, 2021

TMDA, WAHARIRI WAKUTANA ARUSHA KUJADILI SHERIA YA DAWA NA VIFAA TIBA NCHINI

NA MWANDISHI WETU

WAHARIRI wa vyombo vya habari na waandishi nchini wamepongezwa kwa kuwa mstari wa mbele wakitoa taarifa mbalimbali kuhusu umuhimu wa kudhibiti bidhaa unaofanywa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) na hivyo kuongeza tija na uelewa wa Jamii.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bi. Vones Oisso wakati akitoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo ya kikao kazi cha Wahariri na  waandishi wa habari  kutoka Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba, Sura 219.

Bi. Vones Oisso ameeleza kuwa, kikao kazi hicho ni kielelezo tosha kuwa TMDA inatoa kipaumbele kwa masuala yanayohusiana na usalama, ubora na ufanisi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi na pia hivi karibuni, Mamlaka hiyo itaanza udhibiti wa bidhaa zitokanazo na tumbaku.

"Serikali ya Tanzania katika jitihada za kuboresha utoaji huduma katika miaka ya 1990 ni kuanzishwa kwa wakala mbalimbali, Mamlaka ya Dawa na Vifaa (TMDA) ikiwa ni mojawapo.

Sote ni mashahidi wa umuhimu wa Taasisi hii hususan katika kipindi hiki cha majanga ya dunia ya milipuko ya magonjwa kama CORONA na mengineyo mengi". Alisema Bi. Vones Oisso.

Aidha alibainisha kuwa, bila kuchukua hatua za kuhabarisha umma dhidi ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi ni bidhaa nyeti zinazoweza kuwa na madhara makubwa ya kiafya kwa watumiaji kama vile kusababisha ulemavu, kupoteza maisha na kudhoofisha uchumi wa nchi kama hazikudhibitiwa ipasavyo.

Kwa mantiki hiyo bidhaa hizo zinahitaji kudhibitiwa kwa utaratibu wa namna ya pekee; lengo likiwa ni kuzuia madhara ya aina hiyo kwa walaji. Alisema. Bi. Venes Oisso.

Aidha, alipongeza TMDA kwa jukumu la kudhibiti matangazo ya bidhaa za dawa, vifaa tiba na vitendanishi ili kuzuia matangazo yenye nia ya kupotosha umma kwa lengo la kibiashara ambapo matangazo ya aina hiyo hutolewa katika vyombo vya habari.

"Kudhibiti matangazo ni la kisheria na katika kuhakikisha utekelezaji wake, zipo Kanuni za Udhibiti wa Matangazo ya dawa zilizoandaliwa chini ya Sheria Sura 219 tangu mwaka 2010. Hata hivyo, kati ya changamoto kubwa ambazo TMDA imekuwa ikikabiliana nazo toka kuanzishwa kwake ni kushuhudia kutolewa kwa matangazo ya bidhaa inazozidhibiti kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwa ni pamoja na mitandao ya kijamii bila kibali cha TMDA ambapo ni kinyume na matakwa ya Sheria na Kanuni na hivyo kuchangia kupotosha jamii". Alisema Bi. Venes Oisso.

Ambapo amewaomba kuzingatia umuhimu wa michango na kujadiliana kwa pamoja na kutoa maoni ambayo yataisaidia TMDA katika kuboresha huduma zake na hivyo kufanikisha lengo kuu la kulinda afya za jamii.

Pia amewaomba Wahariri hao kuendelea kutumia vyombo vyao vya habari kuwaelimisha wananchi kuhusu suala la dawa bandia  hususan kuwaelimisha wafanyabiashara waache mara moja kununua dawa, vifaa tiba na vitendanishi kutoka maeneo yasiyo rasmi na pia  katika maeneo ambayo ni kinyume cha Sheria kwani mara zote bidhaa hizo huwa si salama kwa matumizi ya walaji.

Aidha, Bi. Venes Oisso alisema Serikali haitamwonea huruma mtu yeyote atayepatikana na bidhaa duni au bandia kwa kigezo kuwa hawakujua wakati huo huo wakiwa wamesababisha madhara kwa watumiaji.

Katika tukio hilo, Maafisa wa TMDA waliweza kuwasilisha mada mbalimbali juu ya shughuli wanazofanya katika Kanda zote hapa nchini ikiwemo bidhaa zisizo na ubora zinavyoweza kuleta athari kwa Jamii.

Pia viongozi wakuu akiweno Mkurugenzi Mkuu wa TMD, Wakurugenzi na watumishi wa TMDA Kanda hiyo ya Kaskazini.

No comments:

Post a Comment

Pages