June 03, 2021

KITS yatekeleza agizo la Rais Samia kuhamasisha uwekezaji nchini



Mkurugenzi Mtendaji wa The Pilgram Group, Miguel Pilgram, ambaye ni mwekezaji katika sekta ya utalii akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo Juni 3, 2021. Wa pili kulia Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Affinity Travel Group, Roslyn Parker, Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii, Jaji mstaafu, Thomas Mihayo na Afisa Kilimanjaro Francis Malugu. (Na Mpiga Picha Wetu).


Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Affinity Travel Group, Roslyn Parker, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo Juni 3, 2021. kwa ajili ya ziara ya utalii na uwekezaji. Katikati ni Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii, Jaji mstaafu, Thomas Mihayo na Meneja Mauzo na Masoko wa Kampuni ya Kilimanjaro International Tourism and Safaris (KITS), Francis Malugu.


Meneja Mauzo na Masoko wa Kampuni ya Kilimanjaro International Tourism and Safaris (KITS), Francis Malugu, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ujio wa wawekezaji katika sekta ya utalii.

 


Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii, Jaji mstaafu, Thomas Mihayo, akizungumza na waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam mara baada ya kuwapokea wawekezaji katika sekta ya utalii.

 

Dar es Salaam, Tanzania

 

 KAMPUNI ya kimataifa inayojihusisha na masuala ya utalii ya Kilimanjaro International Tourism and Safaris (KITS), imekuwa balozi mzuri na lango la kuingiza watalii na wawekezaji nchini Tanzania kutoka majimbo yote 50 ya nchini Marekani ambapo kwa sasa wameleta wawekezaji wakubwa ili kuhamasisha uwekezaji ndani ya mipaka ya nchi yetu.

 

 Akizungumzia kuhusu hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa KITS, Bi. Vonnie Kiondo, alisema hatua hiyo imefikiwa ili kutekeleza azma ya Serikali ya kuongeza na kuboresha mahusiano ya kimataifa, kukuza uwekezaji na utalii hivyo wameleta wafanyabiashara wakubwa wawili kutoka Marekani kwa ajili ya kuitembelea Tanzania na kujionea fursa za utalii na uwekezaji zinazopatikana nchini.

 
Bi. Vonnie ambaye ni mmiliki wa Kampuni hiyo, yenye makao makuu yake jijini Washington DC, Marekani na ofisi za uendeshaji zilizopo Njiro, Arusha, aliwataja wafanyabiashara hao wakubwa ambao KITS imeratibu safari zao kuwa ni Bi. Roslyn Parker, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Affinity Travel Group na Bw. Miguel Pilgram ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa The Pilgram Group. 

 

Wageni hawa waliofika Juni 3 mwaka huu wanatarajia kuondoka nchini Juni 11 mwaka huu baada ya kufanya mikutano ya uwekezaji katika sekta ya utalii ambapo wamepokelewa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kwa mazungumzo maalumu baina ya wawekezaji hao na uongozi wa TTB pamoja na wawakilishi wa mamlaka nyingine za Serikali zikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Maliasili na Utalii na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

 Alisema katika ziara hii wageni hao watakutana na wasanii mbalimbali wa sanaa za muziki na ubunifu wa mavazi  katika kuona namna ambavyo wasanii wanaweza kupata soko la bidhaa zao katika nchi ya Marekani. Wageni hao watapata pia fursa ya  kutembelea jiji la Dar es Salaam, maeneo ya kihistoria Bagamoyo pamoja na visiwa vya  Zanzibar.

 

 "Tunatarajia ziara hiyo kuwa na faida kubwa na miongoni ni kuuza na kutangaza kazi za  wasanii na wanamuziki wetu ughaibuni nchini Marekani hasa kutokana na ushirikiano wakibiashara unaotarajiwa kuanzishwa." Alisema na kuongeza kuwa, "Tunatarajia ziara hiyo iweze kuongeza ajira miongoni mwa Watanzania, ichochee kuongezeka kwa mapato ya kiuchumi katika sekta mbalimbali zinazohusiana na utalii na ukarimu ikiwa ni pamoja na kuuzwa nje kwa kazi za wasanii, bidhaa za mitindo na mavazi ya asili.”

Aliongeza kuwa; “Ziara hii itanufaisha Tanzania kwa kupelekea ujenzi na kuletwa nchini kwa mara ya kwanza jina kubwa (mega brand) la hoteli maarufu nchini Marekani na duniani kote na kujengwa kwa malazi ya gharama nafuu katika maeneo mbalimbali ya hifadhi na yanayotembelewa na wageni wengi ikiwemo Dar es Salaam, Zanzibar, Kilimanjaro, na Dodoma ili kufikia lengo la Serikali ililojiwekea la kufikisha jumla ya watalii milioni 5 mwaka 2025 kwa kuweka malazi ya gharama nafuu katika maeneo mbalimbali jambo ambalo litawavutia watalii wengi kutoka  Marekani na nchi nyingine duniani kutembelea Tanzania.
 

Faida nyingine alisema ni kutumia miundombinu ya kibiashara ya kampuni ya KITS, washirika wake wa kimkakati, uhusiano wa kimataifa, pamoja na watanzania kuchangia ukuaji wa uchumi, mitaji na rasiliamali hivyo kutoa wito kwa watanzania  wengine walio nje ya nchi kuchukua jukumu la kuitangaza nchi na kuvutia  mitaji katika sekta mbalimbali hapa nchini.
 

Pia ujio huo utaimarisha mahusiano kati ya kampuni ya KITS na Affinity Travel Group ambao wamekuwa wakipeleka misafara mikubwa ya watalii na wawekezaji wengi kutoka Marekani  kwenda katika nchi nyingine za Afrika, hivyo itegemewe kwa ushirikiano huu Tanzania itatembelewa na watalii na kupata wawekezaji wengi watakaokuja kushiriki katika fursa zinazopatikana nchini.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa wafanyabiashara hao wawili kutoka jimbo la Florida ni zao la KITS kutangaza utalii na uwekezaji nchini Tanzania kwa wamarekani na duniani kwa ujumla kwa kuwaelewesha kwamba Tanzania ndio nchi yenye vivutio bora vya utalii na sehemu salama za uwekezaji barani Afrika. 

 

"Kwa kupitia kampuni ya KITS ambayo ipo nchini Marekani, watalii na wawekezaji wanapata taarifa sahihi, za moja kwa moja na kwa haraka wakiwa bado ndani ya nchi yao kitu ambacho huiamarisha ushindani wa Tanzania dhidi ya nchi jirani zinazopakana nasi zinazotangaza vivutio na uwekezaji kwenda kwenye nchi zao ili kuipiku Tanzania ." alisema Bi. Vonnie Kiondo.


Aliongeza kuwa Kampuni yao ilianzishwa kwa lengo mahsusi la kutangaza vivutio vya Tanzania yote kwa usawa Bara na Visiwani ili kuwezesha kuongezeka kwa ujio wa watalii hapa nchini. 

 

Akizungumzia dhamira kuu ya kampuni hiyo alisema ni kuchangia ukuaji wa uchumi kutokana na kazi wanazozifanya za kuongoza watalii, kuvutia watalii, kutoa utalaamu wa ukuzaji wa biashara hasa ya utalii kwa kutangaza vivutio vya kitalii, kutoa elimu kwa taasisi na makundi mbalimbali pamoja na kuvutia uwekezaji.


Jambo hilo linaweza kuwa faraja kwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ambayo imekuwa ikihamasisha mabalozi na watanzania waishio nje ya nchi kutangaza vivutio vya utalii na uwekezaji.

No comments:

Post a Comment

Pages