September 26, 2021

ACT wagomea kikao cha Msajili wa vyama


Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma, Salim Biman.

 

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Chama cha ACT Wazalendo kimegomea kikao kilichoitishwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa ambao ungekutanisha vyama pamoja na Jeshi la Polisi.

Taarifa ya chama hicho iliyosainiwa na Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano kwa Umma, Salim Bimani mapema leo, Septemba 26,2021 imesema kikao cha Jeshi la Polisi na vyama vya siasa kilichoitishwa na Ofisi ya Msajili kilichopangwa kufanyika Oktoba 21,2021 hakina nia njema na kinaweza kutumika kuhalisha ubinywaji wa haki za kisiasa nchini.

Taarifa hiyo imesema kikao hicho kilipaswa kudhuriwa mahsusi na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwakuwa ndiye mwenye dhamana ya masuala ya kisiasa kwa Jeshi la Polisi.

"Tumepata taarifa kupitia vyombo vya habari kuwa kikao cha Jeshi la Polisi na Vyama vya Siasa kilichoitishwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kimepangwa kufanyika tarehe 21 Oktoba 2021.

"Baada ya tafakuri ya kina, ACT Wazalendo tumeamua kuwa hatutashiyiki kikao hicho kwa sababu zifuatazo;-

"Tarehe 21 hadi 22 Oktoba 2021, viongozi wakuu wa ACT Wazalendo watakuwa kwenye Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa Haki, Amani na Maridhiano ulioitishwa na Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD) ambapo Mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu Samia Suluhu Hassan."amesema Bimani.

Aidha Bimani ameitaja sababu nyingine kuwa ni Baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutangaza kikao cha Polisi na Vyama vya Siasa, Chama Cha ACT Wazalendo kupitia Kiongozi wa Chama Ndugu Zitto Kabwe, kilimwandikia Msajili kuwa kikao hicho kimjumuishe Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye ndiye mwenye dhamana ya kisiasa ya Jeshi la Polisi lakini hadi sasa hawajapata mrejesho wa suala hilo na mwelekeo ni kuwa kikao hicho kitakuwa cha Polisi na Vyama vya Siasa pekee.

Aliongea kuwa matamshi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro baada ya kikao chake na Msajili wa Vyama vya Siasa hayaonyeshi nia njema ya kikao hicho. 


Bimani alisisitiza kuwa kauli ya IGP Sirro kuwa nchini Tanzania hakuna shida kuhusu mikutano ya nje na kwamba tatizo lipo kwenye mikutano ya ndani na inabidi sheria iwekwe sawa ni dalili ya wazi kuwa kikao hicho kinaweza kutumika kubinya zaidi shughuli za kisiasa nchini.

No comments:

Post a Comment

Pages