September 25, 2021

KASI NDOGO UJENZI BARABARA KIDATU-IFAKARA

 

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa (katikati), akifafanua jambo kwa Mbunge wa Kilombero Mhe. Abubakar Asenga walipokutana wakati wa kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Kidatu-Ifakara ambayo ujenzi wake unaendelea (kulia), ni Meneja wa Wakala wa Barabara TANROADS Mkoa wa Morogoro Eng. Baraka Mwambage.

Muonekano wa nguzo za daraja jipya la Kilombero mkoani Morogoro ambalo ujenzi wake unaendelea.

 

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa ameelezea kutoridhishwa kwake na kasi ya ujenzi wa barabara ya Kidatu - Ifakara yenye urefu wa Km 66.9 inayojengwa na Mkandarasi Reynolds Construction Company (RCC), toka Nigeria.

Kufuatia hali hiyo amemuamuru Meneja Mradi wa Ujenzi huo, Bw. Edan Tesfir kuondoka katika eneo la kazi ili kupisha wataalam wengine kufanyakazi.

Ujenzi huo wa barabara kwa kiwango cha lami pia unahusisha madaraja makubwa matano ulianza mwaka 2017 na ulitarajiwa kukamili mwezi Oktoba mwaka huu lakini hadi sasa umefikia asilimia 37.5 hali inayoonesha hautakamilika kwa wakati.

"Tanroads Mkandarasi hana spidi ya kumaliza mradi huu hivyo hakikisheni mnazingatia mkataba ili haki itendeke na watakaoshindwa kazi waondolewe, wananchi wanataka barabara," amesema Prof. Mbarawa.

Amesema barabara hiyo ambayo ni sehemu ya barabara kuu inayoanzia Dumila- Kilosa- Mikumi -Kidatu  hadi Ifakara itakapokamilika itaunganisha mkoa wa Morogoro na mikoa ya Njombe na Ruvuma na hivyo kuhuisha uchumi wa mikoa hiyo na taifa kwa ujumla.

Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amemtaka mkandarasi anayejenga barabara ya Rudewa-Kilosa Km 24 kuongeza kasi.

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Morogoro Eng. Baraka Mwambage amesema wamejipanga kuwasimamia kikamilifu wakandarasi mkoani humo ili kuepusha adha kwa wasafiri wakati wa mvua.

Naye Mbunge wa Kilombero, Mhe. Abubakar Asenga amepongeza hatua ya ufuatiliaji wa karibu unaofanywa na TANROADS na kusisitiza kuwa wananchi wanaisubiri kwa hamu barabara hiyo ili kuhuisha shughuli za kilimo, uvuvi na biashara.

Zaidi ya shilingi bilioni 100 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi huo ambazo ni ufadhili toka nchi za Umoja wa Ulaya, USAID na UKAID.


 

 

No comments:

Post a Comment

Pages