September 23, 2021

Mtambo achangia ujenzi zahanati ya kijiji Dondo


Aliyekuwa mgombea Ubunge Jimbo la Mkuranga Mkoa wa Pwani kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Mhandisi Mohamed Mtambo akikabidhi Sh 250,000 kwa  Mwenyekiti wa Kijiji cha Dondo Wilaya wa Mkuranga mkoani Pwani, Omary Seif Matope (wa tatu kushoto) ikiwa ni sehemu ya ahadi yake ya Sh 500, 000 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho.

 

Na Mwandishi Wetu, Mkuranga

Aliyekuwa mgombea Ubunge wa Jimbo la Mkuranga mkoani  Pwani mwaka 2020 kupitia ACT Wazalendo, Mhandisi Mohamed Mtambo  amechangia Shilingi 500,000 za ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Dondo.

Mhandishi Mtambo alitoa msaada huo baada ya kuombwa na wananchi wa Kijiji cha Dondo, Kata ya Dondo Tarafa ya Kisiju Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani mwishoni mwa wiki iliyopita akiwa kwenye ziara ya kushukuru wananchi kwa kumpigia kura nyingi katika Uchaguzi mkuu uliopita 2020.

Alisema suala la kuchangia, kuhamasisha maendeleo lisihusishwe na itikadi zozote za kisiasa kwa sababu changamoto za wananchi hususan suala la matibabu halichagui nani ataugua na wakati gani.

" Nimekuja hapa kuwashukuru kwa kunipigia kura mwaka jana 2020, nimeona si haki kuwakimbia kwakuwa hatukushinda, nialikeni kwa shughuli zozote za kijamii zikiwemo hitima, harusi, hata kuchimba mitaro ya ujenzi wa zahanati yetu nitakuja.

"Uzalendo kama lilivyo jina la chama chetu ni  pamoja na kurudi kutoa shukrani, kuishi na watu kidugu, kuwaunganisha na si kuwagawa" alisema Mhandisi Mtambo.

Awali akitoa kero ya changamoto ya ukosefu wa huduma za afya kijijini hapo,  Maganga Lugutu alisema licha ya wananchi kujua umuhimu wa kuwa na zahanati, hali ngumu ya uchumi waliyo nayo inawakwamisha kufikia lengo hilo.

"Changamoto kubwa tuliyo nayo kwa sasa ni kukosa huduma ya matibabu, mtu akiugua ni kazi kubwa kuweza kufika hospitali, kwa mfano umbali wa kutoka hapa Dondo hadi hospitali ya Wilaya ya Mkuranga kwa usafiri wa pikipiki ni Sh 10,000 kwenda tu, bado dawa, vipimo na mgonjwa akilazwa shida inakuwa kubwa zaidi tunaomba serikali ituangalie kwa jicho la pekee kutuongezea nguvu kwani tunateseka sana kwa kukosa zahanati" alisema Lugutu.

Akipokea sehemu ya mchango huo kwa niaba ya Kamati ya ujenzi wa zahanati hiyo,  Mwenyekiti wa Kijiji cha Dondo, Kata ya Dondo Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Omary Seif Matope, alisema kata hiyo haijawahi kuwa na zahanati tangu Tanzania ipate uhuru wake mwaka 1961.

Alisema licha ya Kata hiyo kuwa na idadi kubwa ya watu, shule moja ya msingi na sekondari wamekuwa wakifuata matibabu kwenye kata zingine ambazo zipo umbali mrefu na kijiji chao.

Matope alishukuru mchango huo wa fedha uliotolewa na Mgandisi Mtambo akisema utawasaidia kwenye ujenzi huo wa zahati.

"Hadi sasa wananchi kwa nguvu zetu tumeweza kufyatua tofari 2800 huku mahitaji yakiwa ni tofari 10500 hadi kukamilisha boma lote...., kwa niaba ya wananchi wa Dondo namshukuru huyu kijana wetu kwa kutushika mkono, ni rai yangu niombe wengine waige mfano huu wa kujitoa kwa ajili ya wengine.

"Kama mwenyewe alivyosema, maendeleo hayana chama, kwanza huu si muda wa kampeni, hatuna uchaguzi wowote hapa bali Dondo, kijana wetu ameguswa na changamoto hii kama mtanzania yeyote na si vinginevyo " alisema Matope.

No comments:

Post a Comment

Pages