September 23, 2021

BASATA, Mashirikisho ya Sanaa kufanya Mkutano Mkuu wa Sekta ya Sanaa Septemba 29 Dar

 

Kaimu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Matiko Mniko akizungmza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam kuhusu Mkutano Mkuu wa Sekta ya Sanaa Tanzania utakaofanyika jijini humo Septemba 29 mwaka huu.

 

Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi nchini Adrian Nyamangalle akizungumza na vyombo ya habari leo jijini Dar es Salaam kuhusiana na mkutano huo utakaofanyika Septemba 29 mwaka huu.

 


 

Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Mzee Yusuf akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu ushiriki wa shirikisho hilo katika mkutano huo utakaofanyika Septemba 29 mwaka huu.


Rais wa Shirikisho la Sanaa za Maonesho Tanzania, Cynthia Henjewele akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam kuhusu Mkutano Mkuu wa Sekta ya Sanaa utakaofanyika katika Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa Septemba 29, Dar es Salaam.

 

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam


Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kushirikiana na Mashirikisho ya Sanaa nchini linatarajia kufanya Mkutano Mkuu wa Sekta ya Sanaa Tanzania utakaofanyika Septemba 29 mwaka huu katika Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa, jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa leo jijini humo na Kaimu Mtendaji wa Baraza hilo Matiko Mniko wakati akizungumza na wanahabari kuelekea mkutano huo ambao hufanyika kila mwaka ukiwashirikisha wadau mbalimbali wa sanaa.

Amesema kuwa lengo la mkutano huo ni kujadili masuala mbalimbali yahusuyo sekta ya sanaa  na kwamba ni jukwaa muhimu litakalosaidia kuboresha tasnia hiyo kuifanya iwe rasmi na kuendeshwa kibiashara.

" Lengo kuu la Serikali ni kuifanya sanaa  iwe rasmi iendeshwe kibiashara tutajadili mambo mbalimbali zikiwemo changamoto zinazoikabili tasnia ya sanaa pamoja na yatakayofanikisha kazi zao kutambulika," amesema Mniko.

Amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inatambua mchango wa sanaa kwani imeanzisha Mfuko Maalum wa Sanaa ukitengewa Sh Bilioni 1 zitakazotumika katika kutoa mafunzo na kutoa mikopo kwa wasanii wa tasnia mbalimbali.

Amesisitiza kuwa mkutano huo umebeba kauli mbiu isemayo Sanaa Biashara huku akiongeza utahudhuriwa na wataalamu kutoka vyuoni na wafanyabiashara wa tasnia hiyo hivyo amewaomba wasanii na wananchi kuhudhuria kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha sekta ya sanaa nchini.

kwa upande wake, Rais Shirikisho la Muziki Nchini ambaye pia ni muimbaji wa muziki wa Taarab, Mzee Yusuph amesema mkutano huo utasaidia kutoa majibu ya maswali wanayoulizana wasanii hivyo amewahimiza kuchangamkia fursa hiyo na kuacha kuongea mitandaoni badala wahudhurie ili wachangie mawazo yatakayoleta tija kwenye tasnia ya sanaa.

Nae, Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Elia Mjata ameipongeza kulishukuru BASATA kwa kuwashirikisha kuhudhuria mkutano huo na kwamba wasanii wajikoteze kujadili na kutatua changamoto lengo ikiwa kuifanya sanaa iwe biashara.

Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi, Adrian Nyamangalle amefafanua kuwa mkutano huo utasaidia kubadilisha mtazamo hasi waliyonayo watu kuwa sanaa ni anasa na badala yake utawafanya watambue kuwa sanaa ni burudani, ajira na biashara.

Rais wa Shirikisho la Sanaa za Maonesho Tanzania, Cynthia Henjewele amesema mkutano huo utaleta tija kwa kujadili changamoto zinazoikabili sanaa ikiwemo sanaa hizo na kuwajenga wasanii kuifanya kua biashara.

No comments:

Post a Comment

Pages