September 20, 2021

MAZEMBE YAIONYESHA SIMBA PANAPOVUJA



Na John Marwa


MABINGWA mara tano wa Ligi ya Mabingwa Afrika CAF CL, TP Mazembe waetibua sherehe za tamasha la Simba Day 2021 baada ya kuondoka na ushindi wa bao (1-0).


Mazembe walikuwa wageni katika makala ya 13 Simba Day, ambapo wekundu wa Msimbazi hutumia tukio hilo kila mwaka kutambulisha kikosi cha msimu husika ulioko mbele yao.


Ulikuwa mchezo wa haja sana ndani ya dakika 90 zilizotosha kukata kiu ya burudani ambayo wapenzi na mashabiki wa Soka waliitarajia kuiona kutoka kwa Mabingwa wa Nchi Simba SC.


Hadi dakika ya 84 ngoma ilikuwa ngumu kwa pande zote mbili kabla ya safu ya ulinzi ya Simba kufanya kosa moja na Mazembe kutumia kosa hilo kuwahukumu.


Dakika moja baadae Ousmane Sakho alishindwa kuisawazishja Simba baada ya kupata nafasi ya wazi. Dakika 90 zikatamatika kwa Mnyama anashindwa kuwapa furaha mashabiki zake.


Licha ya kichapo hicho unaweza kusema Simba walifanikiwa sana kwa kupata ushindani halisia wa Ligi ya Mabingwa Afrika kuelekea msimu mpya wa 2021/2022.


Ukiwatazama wachezaji wa Simba ambao ni maingizo mapya walikuwa na kiwango bora sana kuanzia kwa kiungo wa ulinzi Saido Konoute, Ousmane Sakho, Dancan Nyoni, Peter Banda na Kibu Denis.


Je bila Chama na Miquissone Simba ni ya moto ama baridi ? Hili mashabiki walitarajia kuona kama mapengo yao yameziba. Ukweli ni kwamba maingizo mapya yanaileta Simba mpya hasa katika namna ya kucheza hivyo wanahitaji muda wa kutosha kuthibitisha hilo japo bila shaka ni wachezaji walio timia.


Ni wapi panapavuja hapa Didier Gomes Da Rosa nawasaidizi wake wanayo kazi ya kuiunganisha safu ya kiungo cha ushambuliaji na safu ya ushambuliaji sehemu pekee ambayo ilionyesha inahitaji bado kuwa hatari zaidi.


Tukuziacha dakika 90 za uwanjani lilikuwa tamasha lililofana sana mwaka huu kwa burudani nyingine zilizotangulia amabazo zilishereheshwa na wasanii mbalimbali ambao ni mashabiki wa Simba.


Kikosi cha Simba sasa kinaingia mawindoni kujiwinda na mchezo wa Ngao ya Jamii September 25 dhidi ya watani zao wa Jadi Yanga SC, mtanange utakaolindima katika Dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. 

No comments:

Post a Comment

Pages