September 18, 2021

Yanga yaungana na TTB kutangaza utalii wa nchi mechi ya Rivers United

 



Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

Klabu ya Yanga imesema imeingia makubaliano na Bodi ya Utalii Nchini (TTB) kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kutangaza utalii wa nchi kwa kuvaa Jezi zenye nembo ya VISIT KILIMANJARO & ZANZIBAR katika mechi za hatua za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo Haji Mfikilwa wakati akitoa taarifa kwa wanahabari kuhusu makubaliano hayo na kuelekea mchezo wa marudiano dhidi ya Rivers United ya Nigeria utakaochezwa Jumapili nchini humo.

Amesema kuwa wameaumua kuungana na  Bodi ya Utalii nchini (TTB) kupitia Wizara hiyo kutangaza utalii kwa kuunga mkono juhudi za Serikali kuinua sekta hiyo kuongeza mapato ya nchi hivyo watatumia fursa ya mechi hiyo kutangaza vivutio vya utalii.

" Klabu haijapokea fedha yeyote kutoka Serikalini  tumeamua kuungana na TTB kusapoti utali wetu tunaunga mkono juhudi za serikali kukuza utalii wetu, ni juhudi ya kila mtu kuuutangaza," amesema Mfikilwa.

Amebainisha kuwa wataanza kutangaza utalii kupitia mechi hiyo na kwamba kwenye jezi watayovaa itawekwa nembo ya maneno hayo upande wa bega la kushoto la jezi ya Yanga.

Kwa upande wake, waziri wa wizara hiyo, Dkt, Damas Ndumbaro amesema klabu hiyo imevunja rekodi kwa kuwa klabu ya kwanza kuunga mkono kampeni ya Royal Tour ya kutangaza utalii wa nchi inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Ameishukuru klabu ya Yanga kwa kukubali kutumia nembo hiyo bila gharama yeyote kwani kama ingehitaji fedha zaidi ya Sh bilioni moja huku akipendekeza kuwekwa utaratibu baada ya mechi ya watani wa jadi kutembelea vivutio vya utalii.

Ameongeza kuwa anaamini wanaenda kubadili matokeo katikamechi hiyo ya marudiano na ikivuka raundi ya pili ya mashidano hayo nembo hiyo itawekwa upande wa mbele wa jezi ya Yanga.

Nae, Mweyekiti wa Bodi hiyo, Jaji Thomas Mihayo ameishukuru Yanga kwa kuungana na TTB kutangaza utalii wa Tanzania Bara na Visiwani na kwamba sekta hiyo huingizia nchi asilimia 17% ya pato la taifa.

Aidha, amesema kusingekuwa na Ugonjwa wa Corona mwaka jana nchi ingepokea watalii milioni mbili na kuiombea klabu hiyo ivuke raudi inayofuata ili iendelee kutangaza utalii wa nchi.


No comments:

Post a Comment

Pages