September 30, 2021

RC Makalla apokea malalamiko kelele nyumba za ibada, atoa mwongozo

 



Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla ameitaka Idara ya Mipango Miji kufanya kazi karibu na viongozi wa dini ili kuwapanga na kupunguza kelele.

Ameeleza hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua warsha iliyowakutanisha Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Viongozi wa dini Mkoa wa Dar es Salaam.

Amesema katika ziara yake aliyoifanya katika majimbo 10 amepokea kero 927, ambapo 345 zikiwa za ardhi, zikifuatiwa na miundombinu, mirathi pamoja na kelele.

Amebainisha kuwa malalamiko yaliyohusu kelele yalikuwa 85 na kati ya hayo 65 ni kumbi za starehe na 20 yalihusisha nyumba za ibada.

"Jana (juzi) niliagiza operesheni ifanyike kwa baa na kumbi za starehe maana zimekuwa kero sana, ila kwa nyie tumeamua kutumia njia nzuri ili kuwaita hapa kwa sababu viongozi wa dini ni watu mnaoheshimika sana. Kwa hiyo baada ya mawasilisho yote mjitafakari tulipojenga makanisa au msikiti ni sehemu sahihi?”

"Lakini pia mambo matatu lazima yafanyike..., elimu lazima iendelee kutolewa, mamlaka za Serikali katika halmashauri hasa idara ya mipango miji inatakiwa ifanye kazi karibu na jamii zetu, ili kuwapanga vizuri lakini pia sheria na taratibu zilizowekwa ziendelee kufuatwa," amesema Makalla.

Kwa upande wake, Mkurugenzi mkuu wa NEMC, Dk Samwel Gwamaka amesema  warsha hizo ni mwendelezo wa kutoa elimu ya mazingira kwa umma kwa kuzingatia kanuni ya kelele na mitetemo ya mwaka 2015.

"Leo tumeona tuwaite hapa ili kukuza uelewa athari za kiafya na kijamii zinazotokana na kelele pamoja na kupata maoni yenu. Tunaamini baada ya hii warsha tutapata nafasi ya kuielimisha jamii ambao wengi wao ndio waumini wenu," amesema Dk Gwamaka.

No comments:

Post a Comment

Pages