September 18, 2021

Seikali yaboresha Kiwanja cha Ndege cha Mwanza kimkakati

 

Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Mwanza, Bw. Paschal Kalumbete (kushoto) akimweleza Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mwita Waitara masuala mbalimbali ya kiwanja hicho.


Na Mwandishi Wetu, Mwanza

 

SERIKALI imewekeza kimkakati kwenye Kiwanja cha Ndege cha Mwanza, baada ya kuongeza urefu wa barabara ya kutua na kuruka ndege kutoka mita 3,300 hadi mita 3,800, ili kuruhusu ndege kubwa kutoka mataifa mbalimbali ziweze kuruka na kutua bila tatizo.

Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Sekta ya Uchukuzi), Mh. Mwita Waitara alipofanya ziara ya kikazi kwenye kiwanja hicho, ambapo pia amesema kumejengwa kituo cha umeme wa dharura kilichofungwa majenereta ya kisasa, ambayo yanatumika endapo umeme wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) ukikatika au kuwa mdogo kazi na huduma zinaendelea bila kuathirika.

“Hapa kuna umeme wa uhakika pamefungwa mitambo ya kisasa hata kama umeme wa Tanesco ikitokea umekatika au kupungua tunajenereta ili wakati wote huduma ziweze kupatikana kwa sababu usafiri wa anga ni usafiri wa kimataifa, ukifanya kosa hapa Mwanza umeathiri nchi nzima na unawajibishwa Kimataifa na Shirika la Kimataifa la Anga, linafuatilia kwani lazima huduma zikidhi vigezo hivyo,” amesisitiza Mh. Waitara.

Kiwanja hicho kimefungwa majenera makubwa manne ya kufua umeme wa dharura, ambapo mawili yanaukubwa wa KvA 650, huku mengine ni KvA 400 na KvA 350.

Pia amesema kiwanja hicho kimefungwa taa za kumuongoza rubani kutua na kuruka  nyakati za usiku, ambapo kumekuwa na usalama.

Hata hivyo, Mh. Waitara amesema serikali inaendelea kununua ndege hivyo ni lazima kuwe na viwanja vinavyofanya kazi saa 24, pia kuwe na umeme wa uhakika, rada za kuongoza ndege na mitambo ya kisasa ya utabiri wa hali ya hewa, ambapo kutasababisha kuongezeka kwa ndege, watalii na pato la taifa.

Halikadhalika, Mh. Waitara amesema serikali imeboresha usalama kwenye viwanja vya ndege wa kufunga rada ya kisasa, ambazo zinawakikishia watoa huduma kuwa anga la Tanzania ni salama wakati wote.

Lakini, amewakumbusha mamlaka zote zinazohusiana na usafiri wa anga kuwa serikali imewekeza kwa lengo la kukusanya mapato, ambapo sasa anga ni fedha kutokana na ndege zote zinazoingia nchini au kupita kwenye anga la Tanzania zinalipia tofauti na zamani.

Naye Meneja wa Kiwanja hicho, Bw. Paschal Kalumbete amesema serikali ipo katika hatua za mwisho ili kukifanya kiwanja hicho kuwa cha kimataifa kutokana na kuwa na miundombinu ya kisasa.

“Serikali imewekeza miundombinu ya kisasa mfano kumewekwa majenereta makubwa yenye uwezo wa kupokea, kufua na kusambaza umeme ambapo kunatoa uhakika wa huduma zinaweza kutolewa kwa saa 24 bila kujali kunapokuwa na changamoto za umeme,” amesema Bw. Kalumbete.

Pia amesema “ili uweze kushindana kimataifa, inapaswa kuhakikisha kuwa viwango vya usalama kiwanjani kwako viko juu kwa mfano uwepo wa rada unaboresha usalama kwa usafiri wa anga kwani inawawezesha waongoza ndege kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa pasipo kusababisha ajali”

 

No comments:

Post a Comment

Pages