Farida Ramadhani, WFM, Dodoma
Serikali imetoa wito kwa Benki ya NMB kubuni huduma ambazo zitakidhi mahitaji ya wananchi kulingana na mabadiliko ya mazingira.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Benki hiyo ofisini kwake jijini Dodoma.
Tutuba alisema, mazingira yamekuwa yakibadili na mahitaji ya wananchi nayo yanabadilika kulingana na mazingira hivyo ni vyema benki hiyo iongeze jitihada za kukabiliana na mambo hayo ili kuwafikia wananchi na kuendelea kufanya vizuri katika soko.
“Na sisi kama Serikali tunaahidi kuwa tutaendelea kufanya kazi na nyinyi kwa kuhakikisha tunaweka mazingira mazuri ya kuwezesha Sekta hii ya fedha kukua kwa ustawi “, alisema.
Katibu Mkuu huyo aliitaka Benki ya NMB kuongeza jitihada katika kupunguza mikopo chechefu ambayo ni changamoto ya muda mrefu ingawa amebainisha kuwa baadhi ya mikopo hiyo imekuwa ikisababishwa na benki zenyewe.
“Hili la mikopo chechefu inabidi muwe makini sana katika kutathmini utoaji wa mikopo kwa wateja unakuta mteja hana historia nzuri ya masuala ya kibenki halafu mnamkopesha mnadhani nini kitatokea…”, alihoji Tutuba.
Pia aliiagiza Benki hiyo kuongeza jitihada za kupunguza riba za mikopo kwa wateja wao, changamoto ambayo imekuwa ni ya muda mrefu kwa taasisi za fedha nchini.
Aidha, aliwasihi kuhakikisha wanaikumbuka sekta ya elimu katika shughuli zao za kurudisha fadhila kwa jamii, hususani katika kipindi hiki ambacho Serikali ipo katika jitihada za kuhakikisha inajenga madarasa na madawati ili kuhakikisha wanafunzi wote watakaochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwakani wanasajiliwa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna aliahidi, kuyatendea kazi maagizo yote yaliyotolewa na Serikali na kubainisha kuwa benki hiyo iko tayari kushirikiana na Serikali wakati wote.
Alisema benki hiyo iko vizuri kwa sasa katika nyanja tofauti tofauti ikiwemo uwekezaji, uendeshaji, mikopo pamoja na amana ambapo kwa mwaka jana benki hiyo ilipata faida ya Sh. bilioni 206 baada ya kodi na kutoa gawio la Sh. bilioni 68.5 kwa wanahisa wote, huku Serikali ikipata gawio la Sh. bilioni 21.8.
No comments:
Post a Comment