September 23, 2021

WAKAZI CHALINZE KUONDOKANA NA KERO YA MAJI


Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akitoa maelekezo kwa Meneja wa Dawasa Mkoa wa huduma Chalinze Pascal Fumbuka alipokagua mradi huo uliopo Chalinze.


 

Na Julieth Mkireri, Chalinze

WAKAZI wa Chalinze wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani wanatarajia kuondokana na kero ya maji inayowakabili kwa muda mrefu ifikapo mwezi Octoba mwaka huu utakapokamilika mradi wa maji Mlandizi -Mboga.

Hayo yameelezwa jana mjini Chalinze na Meneja wa Mamlaka ya maji safi na maji taka Dar es Salam (DAWASA) Mkoa wa huduma wa Chalinze Mhandisi Paschal Fumbuka wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge kusikiliza kero za wananchi na kukagua miradi.

Mhandisi Fumbuka alisena kukamilika kwa mradi huo kutaondoa kikwazo Cha kukatika kwa maji mara kwa mara kero ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wakazi wa mji wa Chalinze na maeneo ya jirani.

Meneja huyo alisema uwezo wa mitambo iliyopo sasa ni kuzalisha maji mita za ujazo 7500 huku mahitaji yakiwa 15,000.

Aidha alieleza kuwa mradi wa Mlandizi-Mboga utakapokamilika kwa siku utakuwa na uwezo wa kuzalisha maji mita za ujazo 9000 na kuondoa kero iliyokuwepo awali.

Mhandisi Fumbuka alisema hakuna mfanyakazi anayehujumu usambazaji wa maji kwa manufaa binafsi na hivyo aliahidi.kuzingatia maelekezo ya Mkuu wa Mkoa ya kuhakikisha wateja wa majumbani wanapata maji kama ilivyo katika maeneo mengine.

Akikagua mradi huo mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alitoa maelekezo kwa mamlaka hiyo kuhakikisha mradi huo utakapoanza kazi maji yafike kwa wananchi muda wote.

Baadhi ya wakazi wa Chalinze walimueleza Mkuu was mkoa kuwa kukuwa na kero ya upatikanaji wa maji ambapo wakati mwingine wanakaa wiki mbili hadi tatu bila huduma hiyo ya maji ya bomba.
 

No comments:

Post a Comment

Pages