September 04, 2021

WAKULIMA WA MAHINDI SONGEA WALALAMIKIA UNUNUZI WA MAZAO NFRA

 NA STEPHANO MANGO, SONGEA

 

WAKULIMA wa zao la mahindi Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma wameilalamikia Serikali kupitia wakala wa hifadhi ya Taifa (NFRA) Kanda ya Songea kwa kushindwa kununua mahindi yao badala yake wananunua mahindi ya wafanyabiashara wakubwa na viongozi wa kada mbalimbali nyakati za usiku.

 

Wakizungumza mbele ya waandishi wa habari jana nje ya eneo la NFRA Kanda ya Songea kwa nyakati tofauti mjini hapa wakulima hao ambao wameomba majina yao yahifadhiwe walisema kuwa mahindi yao hayanunuliwi kwa kigezo kuwa ni machafu na hayana ubora wakati jambo hilo sio la ukweli.

 

"Awali waliambiwa kuwa  watanunua mahindi toka kwa wakulima gunia 80, baadae wakasema watanunua gunia 50 kwa kila mkulima lakini leo wanasema kuwa watanunua mahindi gunia 10 kwa kila mkulima, sasa huu mkanganyiko unatokea wapi na wakulima tupo hapa kwenye foleni zaidi ya wiki mbili na zaidi ya magunia 100".

 

“ Tunashindwa kuelewa hatima yenu ni ipi katika ununuzi wa mahindi yetu, kila kukicha tunaandikisha majina ya wakulima 20 lakini katika kwenda kupima wakulima 7 tu kati ya 20 ndio wanafanikiwa kupimiwa mahindi yao na 13 waliobaki mahindi yao yanatolewa nje kwa madai kuwa ni machafu, huku tukiwa tunadaiwa fedha za usafiri wa mahindi kutoka vijijini kuyaleta hapa” walisema.

 

Walimeiomba Serikali kuona umuhimu wa kuangalia kwa upana wake suala la ununuzi wa zao hilo kutoka kwa wakulima kwasababu ndio zao pekee kwao na wakati wa msimu wa kilimo ujao unakaribia.

 

Kwa upande wake Meneja wa NFRA Kanda ya Kusini Mohamed Nondo alisema kuwa fedha wanazopokea toka Serikalini ni ndogo, hivyo kadri wanavyopokea ndivyo wanavyonunua, na kwamba kwasasa wanatarajia kununua tani 4000.

 

Nondo alisema kuwa madai mengine yanayotolewa na wakulima hao hayana ukweli wowote na kama kuna mkulima anaushahidi wa jambo hilo basi aupeleke kwenye vyombo vinavohusika ili hatua ziweze kuchukuliwa

No comments:

Post a Comment

Pages