September 28, 2021

Waziri Makamba: Tunataka TANESCO iendeshwe kibiashara

 

Wajumbe wapya wa bodi ya TANESCO.

 

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam


Waziri wa Nishati,January Makamba amesema ni wakati sasa Shirika la Umeme Tanzania TANESCO linatakiwa kuanza kujiendesha kibiashara, kwa ufanisi ili kuchangia uchumi wa Taifa.
 
Ameyasema hayo jijini Dar es Salaam Katika Ukumbi wa kimataifa wa Mkutano wa Mwalimu Nyerere wakati akizungumza na Mameneja wa TANESCO wa ngazi ya Kanda, Mikoa, Wilaya na Makao Makuu. 
 
Aidha Waziri Makamba amewatambulisha Wajumbe wa Bodi ya TANESCO wakiongozwa na Mwenyekiti Omari Issa, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji Maharage Chande, walioteuliwa Septemba 25, 2021 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
 
Wajumbe wa Bodi ya TANESCO waliotambulishwa ni pamoja na  Nehemia Mchechu, Zawadia Nanyaro, Lawrence Mafuru, Mhandisi Cosmas Masawe, Balozi Mwanaidi Maajar, Mhandisi Abdallah Hashim,  Abubakar Bakhresa na  Christopher Gachuma.
 
Mhe. Makamba amesema Bodi iliyochaguliwa ina wajumbe kutoka nyanja mbalimbali na watasaidia Shirika kufikia malengo.
 
 "Tunataka baada ya miaka mitatu Shirika liingie katika orodha ya mashirika bora, yenye thamani na yanayoheshimika Afrika" alisema Mhe. January Makamba
 
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Bw. Omari Issa, amesema atahakikisha Bodi inafanya kazi na kutimiza malengo yake kwa kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa malengo na uwajibikaji.
 
 Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Maharage Chande, ameeleza vipaumbele ambavyo ni masilahi ya rasilimaliwatu, Wateja wa Shirika na utekelezaji wa mipango, hivyo ameomba ushirikiano kutoka kwa wafanyakazi wa TANESCO.
 
"Nimhakikishie Mhe. Waziri tutahakikisha tunarudisha heshima ya Shirika na ufanisi kupitia ushirikiano wenu, hakuna Shirika lolote linalotoa huduma ya umeme zaidi yetu sisi, yamkini tuwape wateja wetu huduma wanayostahili", " alisema Bw. Maharage Chande
 
Meneja Mwandamizi Rasilimaliwatu, Bw. Francis Sangunaa, aliwahakikishia viongozi ushirikiano kwa niaba ya wafanyakazi wa TANESCO.
 

No comments:

Post a Comment

Pages