September 07, 2021

Wizara, taasisi zaagizwa kujiunga huduma pamoja

 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Vituo vya Huduma Pamoja kwenye viwanja vya Posta, Dar es Salaam.

 

Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo akitoa taarifa kuhusu vituo vya huduma pamoja kabla Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa hajazinduzia vituo hivyo kwenye viwanja vya Posta, Dar es Salaam.

 

Viongozi wa Dini wa Mkoa wa Dar es Salaam wakimsikiliza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (hayupo pichani) akihutubia kabla ya uzinduzi wa Huduma Pamoja kwenye viwanja vya Posta, Dar es Salaam.

 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, akizindua Vituo vya Huduma Pamoja kwenye viwanja vya Posta, Dar es Salaam.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Gloria Oshudada, Msimamizi wa Huduma kwa Wateja wa Shirika la Posta Tanzania kuhusu Huduma Pamoja ndani ya Ofisi ya Posta Kuu, Dar es Salaam.

 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza mbele ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (hayupo pichani) kabla ya uzinduzi Huduma Pamoja kwenye viwanja vya Posta, Dar es Salaam.


 

Na Selemani Msuya 

 

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza wizara na taasisi zote za Serikali kujiunga na Vituo vya Huduma Pamoja vinavyosimamiwa na Shirika la Posta Tanzania.

Aidha, Majaliwa ameitaka Wizara ya Fedha kupitia madeni ya wadaiwa wote ili kuhakikisha wanalipa madeni yao jambo ambalo litaimarisha shirika hilo.

Waziri Mkuu Majaliwa aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wafanyakazi wa shirika hilo na wananchi katika uzinduzi wa Vituo vya Huduma Pamoja jijini Dar es Salaam.

Majaliwa amezitaja baadhi ya taasisi hizo kuwa ni Tume ya Ajira, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Maeneo Maalumu ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Alisema maboresho ambayo yamefanywa na shirika hilo yanapaswa kuungwa mkono na Serikali yenyewe hivyo aagiza wizara na taasisi zote zijiunge na vituo vya huduma pamoja ambavyo vinasimamiwa na shirika la serikali.

Majaliwa alisema haingii akilini wizara na taasisi zake kutumia fedha nyingi kusafirisha mizigo na vifurishi vingine wakati Shirika la Posta lipo na linatoa huduma hiyo.

“Natumia nafasi hii kuagiza wizara na taasisi zote za Serikali zijiunge na vituo vua huduma pamoja vya Posta ili kuweza kusafirisha mizigo na vifurushi. Haiwezekani tuendelee kutuma gari za taasisi au wizara kusafirisha vifurushi hivyo.

Pia haikubaliki kuendelea kuyapa mashirika mengine ya posta kutoka nje kusafirisha vifurushi vyao wakati shirika letu lipo hivyo nasisitiza kuanzia sasa ambao hawajajiunga eajiunge.

Alisema Shirika la Posta likitumika vizuri litachochea maendeleo ya kijamii na uchumi hivyo kufanikisha lengo la nchi kufikia uchumi wa viwanda.

Waziri Mkuu alisema uzinduzi huo wa Vituo vya Huduma Pamoja  ni muendelezo wa shirika kuja na huduma bora mbapo awali walizindua huduma ya Posta Kidigitali na Biashara Mtandao ambazo zimeonesha matokeo chanya.

Alisema shirika hilo lilikuwa linasuasua ila kwa kinachooneka kwa sasa kinaakisi lengo la Serikali la kuifanya Tanzania kufikia uchumi wa kati na viwanda.

“Uzinduzi wa mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan yenye kuakisi Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya      mwaka 2020,” alisema.

Majaliwa alisema shirika hilo lina ofisi zaidi ya 350 nchini kote hivyo ni vema taasisi za Serikali, mashirika na sekta binafsi kujiunga na posta ili kupata huduma ya pamoja kwa wakati.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Faustine Ndugulile alisema Serikali imetoa Sh. bilioni 7.8 kwa ajili ya kulifufua shirika hilo ambapo hadi sasa Posta wamepokea Sh. bilioni 3.9 ambazo zimeelekezwa kulifanya shirika kuwa jipya kila mahali.

“Shirika la Posta ni moja ya nguzo muhimu katika kukuza uchumi katika mukatadha huo Serikali imeamua kuwekeza Sh.bilioni 7.8 ambapo hadi sasa tumeshato Sh. bilioni 3.9 ambazo zinaendelea kufanya mapinduzi yanayoonekana sasa,” alisema.

Aidha, alisema shirika hilo limepata dola milioni 150 ambapo kati ya hizo dola milioni 21 sawa na Sh.bilioni 49.5 zitatumika kuboresha Vituo vyas Huduma Pamoja hadi ifikapo mwaka 2025.

Dk.Ngugulile alisema vituo vya huduma pamoja vitasaidia kupunguza foleni ambazo zimekuwa zitokea katika maeneo mengine ya watoa huduma Serikalini.

Alisema maboresho hayo yamewezesha shirika hilo kuweza kushirikiana na mashirika ya Posta zaidi 650,000 duniani.

Waziri huyo alisema mafanikio ya Shirika la Posta yatawezeshwa na Watanzani wenyewe kwa kulitumia kutuma vifurushi na mizigo kupitia vyombo vyao ambavyo ni magari, bajaji na pikipiki.

Kwa upande wake Kaimu Posta Masta Mkuu, Macrice Mbodo alisema Vituo vya Huduma Pamoja ambavyo vimezinduliwa leo na Waziri Mkuu Majaliwa vitahusisha Idara ya Uhamiaji, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), 

Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhaminia (RITA), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Mfuko wa Hifadhi za Jamii (NSSF), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Halmashauri.

Mbodo alisema iwapo wizara na taasisi zote zitafungua vituo vya huduma pamoja Posta ni wazi huduma nyingi wanazotoa zitapatikana kwa urahisi.

Alisema kufungua Vituo vya Huduma Pamoja katika mikoa 10 ambayo ni Dar es Salaam, Unguja, Chakechake, Morogoro, Tanga, Arusha, Dodoma, Mwanza, Kigoma na Mbeya.

 

Alisema uanzishwaji wa huduma hizo mpya umewezesha shirika kuongeza mapato hadi kupata faida zaidi ya Sh.bilioni 3.

Mbodo alisema kupitia huduma ya duka mtandao ambao inasimamiwa na shirika wamefanikiwa kuata zaidi ya Sh.milioni 300.

No comments:

Post a Comment

Pages