HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 01, 2021

Zanzibar, Oman kuendeleza Udugu na Oman

 

Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Ndugu Othman Masoud Othman akizumngumza na Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Balozi Said Salim Al-Sinawi.


Na Mwandishi Wetu, Zanzibar


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema mazingira bora yaliyopo sasa yanatoa fursa muhimu ya kukuza mashirikiano kati ya nchi ya Zanzibar na Oman.

Othman ameyasema hayo leo Septemba 1, 2021 ofisini kwake Migombani Mjini Unguja wakati akizungumza  na Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar, Balozi Said Salim Al-Sinawi.

Othman amebainisha mazingira hayo kuwa ni pamoja na ya kijamii, Serikali ya Umoja wa Kitaifa, na pia fungamano la kihistoria la udugu na utamaduni kati ya Zanzibar na Oman.

Aidha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amebainisha uwepo wa fursa nyengine mpya za Uchumi wa Bluu, nafasi za masomo na Utalii ambazo  zinaweza kuongeza kasi ya maendeleo kati ya nchi mbili hizi.

Kuhusu uhusiano wa asili kati ya Oman na Zanzibar, Othman alisema, 'Zanzibar na Oman imekuwa ni ndugu kutokana na mafungamano ya kale baina ya pande hizi mbili, Oman hapa wana ubalozi wao, wao ndio waanzilishi wa Mahakama ya Qadhi sambamba na nyumba za Makumbusho kabla ya hata Kenya, Uganda na kwengineko Afrika ya Mashariki'

Katika ushauri wake, Makamu huyo wa Rais Othman alitoa wito kwa Serikali ya Oman kuwekeza katika mipango maalum ikiwemo ya vituo vya kukuza taaluma, historia na utamaduni, ili kuendeleza urithi na ukarimu kwa vizazi vijavyo, huku akifahamisha kuwa Serikali ya Zanzibar imefungua milango zaidi ya kufanikisha hayo.

Akiwasilisha salamu kutoka kwa Watu wa Oman, Balozi Al-Sinawi amesema umoja kati ya nchi yake na Zanzibar hautoweza kufifia, kwani unatokana na udugu wa kihistoria, wa asili na zama.

Balozi Al-Sinawi ambaye mbali na mambo mengine alifika kwa lengo la kujitambulisha, amebainisha kuguswa mno na fungamano la asili kati ya nchi mbili hizi, amesema atachukua kila juhudi kuishawishi Serikali ya Oman kukuza mashirikiano na kusaidia maendeleo ya Zanzibar.

Amesema pamoja na Janga la Corona kuathiri mipango mingi ya maendeleo, bado azma iliyopo ni kuona Serikali za Oman na Zanzibar zinaendeleza udugu na mashirikiano, na kufanikisha kasi ya maendeleo baina ya pande mbili hizo.

No comments:

Post a Comment

Pages