October 11, 2021

ACT kutumia chaguzi ndogo kujiimarisha kisiasa


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Chama Cha ACT-Wazalendo kimesema kitatumia chaguzi ndogo za marudio zinazojitokeza kama sehemu ya mapambanao yake ya kisiasa sambamba na kujenga mtandao wa chama.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa  chama hicho, Ado Shaibu katika mkutano wake na waandishi wa habari leo Oktoba 11,2021 ambapo pia ametaja sababu za chama chake kuendelea kushiriki  chaguzi ndogo mbalimbali zinazoitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na ile ya Zanzibar (ZEC).

Ado amesema ACT Wazalendo kimeshiriki kwenye chaguzi za majimbo matano na baadhi ya kata nchini kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni Pamoja na kutoa fursa kwa chama kutetea majimbo na kata ambazo chama kilikuwa kinayaongoza kabla ya wabunge au madiwani wake kufariki dunia au kupoteza sifa za kuendelea kushikilia nafasi zao.

Katibu mkuu huyo ameitaja sababu nyingine kuwa ni kupambana kushinda majimbo na kata ambazo hawakushinda kwenye Uchaguzi mkuu 2020 pamoja na kujenga mtandao wa chama pamoja na kupigania demokrasia kupitia majukwaa ya kampeni.

“Sisi ACT Wazalendo tutatumia chaguzi hizi za marudio kama uwanja wa mapambano, na kauli mbiu yetu iko wazi katika hili, tutapambana tukishiriki na tutashiriki tukipamabana.

‘Kila uchaguzi ni somo kwetu, na katika majimbo na kata nyingi tulizoshiriki  tumeongeza wanachama na kusuka mtandao mpya wa uongozi katika majimbo ya Muhambwe, Buhigwe na Ushetu kwa Tanzania Bara na majimbo ya Konde na Pandani Pemba hivyo tutaendelea kutumia majukwaa ya kisiasa kupigania demokrasia, Tume huru ya Uchaguzi pamoja na Katiba mpya”alisema Ado. 

Mbali na hayo, Ado pia aligusia changamoto mbalimbali zinazoendelea kugubika chaguzi mbalimbali za marudio kuwa ni pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuendelea kula njama kwa kushirikiana na wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi pamoja na wagombea wasiokuwa waaminifu ili kiweze kupita bila kupingwa kwenye majimbo na kata nyingi nchini.

“Mathlani kwenye Jimbo la Ushetu, licha ya vyama 16 vya upinzani kujitokeza kuchukua fomu, lakini ni ACT Wazalendo peke yake kilichoweza kurejesha fomu na kushiriki kinyang’anyiro hicho.

“Chanagamoto nyingine ni NEC kupanga muda mdogo wa kampeni wa wiki mbili hadi tatu ambao hautoshi hasa kwenye majimbo makubwa ya Tanzania bara kupiga kampeni kwenye maeneo yote na kuratibu upatikanaji wa mawakala wa majimbo hayo”alisema Ado.

No comments:

Post a Comment

Pages