October 08, 2021

Washiriki watambia Semina ya Kupinga Ukatili, Rushwa ya Ngono kwa Wanawake

NA MWANDISHI WETU

WANAWAKE na wanachama wa Kikundi cha Sauti ya Jamii Kipunguni, wilayani Ilala jijini Dar es Salaam, wamekiri kunufaika vya kutosha na semina iliyofanyika kupitia 'Mradi wa Miezi Mitatu ya Wezesha Uelewa wa Haki, Zuia Rushwa ya Ngono Ndani ya Jamii.'


Baadhi ya wanawake walioshiriki semina ya Kupinga Ukatili, Rushwa ya Ngono kwa Wanawake wakiwa katika picha pamoja mara baada ya semina hiyo.
  
Semina hiyo iliyofadhiliwa na Woman Fund Trust Tanzania, ililenga kutoa elimu ya kupinga, kupambana na kuzuia vitendo vitendo vya Rushwa ya Ngono kwa wadada wa kazi wanawake na wasichana wenye ndoto za uongozi katika jamii na kisiasa kwa ngazi mbalimbali.

Sauti ya Jamii Kipunguni (iliyoratibu na kuendesha semina hiyo), ni kikundi kilichoanzishwa na wanaharakati ambao ni washiriki wa Semina za Jinsia za TGNP Mtandao, waliotokea Kata ya Kipunguni, kwa lengo la kutetea Haki za Wanawake na kupinga ukatili wa kijinsia, ikiwemo kingono, kisaikolojia, kiuchumi, sambamba na ndoa/mimba za utotoni na mila kandamizi, hususani ukeketaji.

Wakizungumza baada ya semina hiyo, baadhi ya washiriki walikiri kukutana na changamoto mbalimbali na vitendo vya ukatili wa kijinsia, ngazi ya familia na hata kisiasa, ambavyo viliwayumbisha na kuwakwamisha, lakini wanaamini elimu waliyopata inaenda kuwapa ujasiri na mbinu mbadala za kupambana na kutokomeza ukandamizaji dhidi yao.

 Seya Kazadi, mmoja wa washiriki wa semina ya Wezesha Uelewa wa Haki, Zuia Rushwa ya Ngono Ndani ya Jamii.'
 
 

Seya Kazadi, ameitaja semina hiyo Kama mkombozi kifikra miongoni mwa kina mama wenye ndoto za uongozi, na kwamba imemuwezesha kupata Uelewa Mkubwa na anajisikia vizuri zaidi ya alivyokuwa kabla ya kupata mafunzo hayo.

"Unyanyasaji wa kijinsia umekithiri sana katika jamii, na waathirika wakubwa ni sisi wanawake. Tunapotafuna maeneo ya kufanya ujasiriamali ama tunapojitokeza kuomba nafasi za uongozi, maombi ya Rushwa ya Ngono yamekuwa kikwazo.

"Utasikia muombaji anakutamkia, bila mimi huwezi kufanikisha adhima yako ya kupata unachotaka. Lakini kupitia semina hii, washiriki tumepata jibu la namna sahihi za kupambana na tatizo hilo.

"Kuna namba za simu za TAKUKURU (113), ambazo tumepewa kuripoti matukio, lakini tunaweza pia kutumia simu zetu kurekodi ushahidi wa maombi ya Rushwa ya Ngono," alibainisha Stella.

 

Mariam Ngomaitala (kushoto) na Salome Masale wakijadiliana jambo baada ya semina ya Wezesha Uelewa wa Haki, Zuia Rushwa ya Ngono Ndani ya Jamii.'


Naye Mariam Ngomaitala, amesema semina hiyo imemfumbua macho kumuwezesha kutambua madhara yatokanayo na Rushwa ya Ngono na kwamba anaenda kuwa balozi mwema kwa jamii wa elimu aliyopata kupitia semina hiyo.


"Nimejifunza ukubwa wa madhara ya vitendo hivi, na nitatumia elimu hii kuifunza jamii inayonizunguka. Uchaguzi ujao wa 2025 nitaingia nikiwa vizuri kimbinu kuweza kukabili Rushwa ya Ngono, sambamba na kukosa uungwaji mkono kutoka kwa mume wangu, vitu ambavyo vilinikwamisha uchaguzi uliopita wa 2020," alifichua Mariam.
 

Kwa upande wake, Salome Masale, yeye alisema moja ya faida aliyopata kupitia semina hiyo ni kujitambua, na kwamba alipitia magumu mengi katika Uchaguzi Mkuu uliopita ikiwemo kuombwa Rushwa ya Ngono na alipokataa, akajikuta akinyimwa nafasi.
"Kupitia semina hii, nimejifunza namna ya kukabiliana, kuviripoti ama kuviepuka vitendo vya Rushwa ya Ngono. Naamini nikiingia katika uchaguzi ujao, nitakuwa imara kuvishinda na kupata mafanikio bila kuruhusu kuathiriwa na vitendo hivyo," alisisitiza Salome.

No comments:

Post a Comment

Pages