HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 01, 2021

Dk. Kijazi: Tunaweza kufika 100% ya kutabiri hali ya hewa

 

Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi.


Ofisa wa Utabiri kutoka TMA, Rose Senyagwa akielezea utabiri wa msimu wa Novemba 2021 hadi Aprili 2022.

 

Na Irene Mark

VIWANGO vya usahihi wa taarifa za hali ya hewa hapa nchini vinaendelea kuimarika baada ya utabiri wa msimu uliopita wa Novemba 2020 hadi Aprili 2021 kuwa sawa kwa asilimia 94.1.

Kwa mujibu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), usahihi wa viwango vya utabiri kidunia vinatakiwa kuanzia asilimia 70 na zaidi ya hapo.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi amesema kiwango cha usahihi wa taarifa za hali ya hewa kinaweza kuongezeka zaidi pale ambapo msimu husika utatawaliwa na mifumo mikubwa kama Lanina au El Nino.

Alisema hayo alipozungumza na HabariMseto Blog hivi karibuni kabla ya TMA kutoa utabiri wa msimu wa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka ambao ni kuanzia Novemba 2021 hadi Aprili 2022.

Dk. Kijazi ambaye pia ni Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO, anasema inawezekana kutabiri na matokeo yakawa sahihi kwa asilimia 100 iwapo mifumo mikubwa ya utabiri wa hali ya hewa inayotumika ktk utabiri wa mvua za msimu ikiwemo Lanina itakuwa "stable" ingawa nayo ina changamoto zake.

Alisema matumizi ya mifumo hiyo hutegemea zaidi joto la bahari.

“Mifumo mikubwa kabisa ya utabiri kama Lanina inapokuwa "stable"  tunaweza kufikia asilimia 100, hapo sasa tutakuwa vizuri zaidi.

“Tunaweza kufikia asilimia 100 ila sasa changamoto ni kwamba joto la bahari halipo ‘stable’ na kubadilika kwake ndio kunaleta matokeo ya utabiri kwa viwango tofauti.

“Shirika la Hali ya Hewa Duniani linataratibu sheria na kanuni zake, linasema nchi ikiweza kutabiri kwa usahihi kuanzia asilimia 70 basi utabiri huo unaweza kutumika kwa shughuli za maendeeo kwenye nchi husika,” anasema Dk. Kijazi.

Baada ya serikali kuiboresha TMA kwa vifaa vya kisasa zikiwemo rada kwenye vituo vya kikanda, pia imeongeza rasilimali watu wenye taaluma  za juu za hali ya hewa, hivyo viwango vya usahihi wa taarifa za hali ya hewa vinaongezeka kila mwaka.

Katika utabiri huo wa msimu, TMA iliitaja mikoa itakayopata  mvua za chini ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi kuwa ni Kigoma, Tabora, Katavi, Singida, Dodoma, Rukwa, Songwe, Mbeya na Iringa.

Mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara na kusini mwa Morogoro na kwamba nusu ya kwanza ya msimu (Novemba - Januari) vipindi virefu vya ukavu vinatarajiwa kwenye maeneo hayo.

Hata hivyo, ongezeko kidogo la mvua linatarajiwa mwezi Machi, 2022 katika nusu ya pili ya msimu.

No comments:

Post a Comment

Pages