HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 01, 2021

RC MALIMA: ATAKAYESABABISHA UGOMVI WA ARDHI NITAMSHUKIA KAMA MWEWE

 


MKUU wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima ameonya iwapo utatokea ugomvi utakaosababishwa na migogoro ya ardhi katika maeneo ya mipaka ya Tanga na Manyara atawashukia kama mwewe waliosababisha mgogoro huo.


Malima amesema hayo wakati wa ziara ya ujirani mwema aliyoambatana na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere kukagua maeneo ya mipaka ya mikoa hiyo yanayodaiwa kuwa na migogoro ya ardhi.


"Nataka niwahakikishie hakuna ugomvi utakaotokana na mgogoro wa ardhi, na ninaapa kama utatokea ugomvi tutawashukia kama mwewe, hatutaruhusu jambo hilo litokee, haipo.


"Ukitaka kujua kwamba ugomvi huu unatengenezwa na watu kwa maslahi yao ni mambo kama hayo, tumetembelea sehemu zote hadi leo hatujaona watu wanagombea mpaka," amesema Malima.


Kwa upande wake Makongoro amesema mipaka haiondoi Utanzania licha ya mwingiliano wa huduma za kijamii isipokuwa ni mambo ya takwimu kwamba sensa ikifanyika watu wajue idadi yao katika eneo wanalotaka suala ambalo ni la utawala na haimzuii mfugaji kupeleka mifugo yake upande wowote.


"Sisi tunaweza kuwa na majina fulani, tunaweza kuwa na dini fulani lakini kitu kinachotuunganisha sisi wote ni Watanzania,"


Naye Mbunge wa Simanjiro, ambaye ni mwakilishi wa wananchi katika zoezi hilo, Christopher Ole Sendeka, amewapongeza wakuu hao wa mikoa kwa hatua hiyo kwani wananchi wamefahamu kuwa hayo ni maeneo tu ya kiutawala lakini wote ni Watanzania na yeyote anaruhusiwa kuishi popote na akawa haki zote ambazo Mtanzania anastahili kupata.


"Nawaomba wananchi muendelee kuwa watulivu mkisubiri maelekezo ya viongozi wetu watakayotoa baada ya kumaliza zoezi hili," amesema.


Ziara ya wakuu hao ya siku mbili ilianza Oktoba 30-31, katika maeneo ya Kitongoji cha Muheza Kijiji cha Leshata ambapo alama inayokutanisha Mkoa wa Morogoro katika kijiji cha Leshata  Wilayani Gairo na Mkoa wa Tanga katika Kijiji cha Chamtui.


Sehemu nyingine ni katika Kilima cha Ngaiyaki wilayani Gairo inayopakana na Wilaya ya Kilindi kijiji cha Chamtui na eneo aambalo mikoa mitatu inakutana yaani Tanga, Manyara na Morogoro kwa Wilaya za Kilindi (Kijiji cha Maslei), Kiteto (Kijiji cha Olgira) na Gairo ( Kijiji cha Leshata).


Aidha, ziara hiyo pia ilipitia katika safu ya Milima Bokwa ambapo Mlima Lengatei na Mlima Mkama unaonekana kwa mbali,   Kijiji cha Mafisa na Kijiji cha Lembapul kwenye alama iliyowekwa yenye kuonyesha mwisho wa mpaka wa Wilaya ya Kilindi na Kiteto na ziara hiyo ukihitimishwa kwenye alama ya upimaji inayotambulika kama Sumatek Trig Point iliyopo juu ya Kilima cha Sumatek inayotenganisha vijij vya Wilaya za Simanjiro na Kilindi.

No comments:

Post a Comment

Pages