January 26, 2022

Dk.Gwajima: Ukatili haukubaliki kwa mtu yoyote

* Watoto wa kike ni waathirika wakubwa wa vitendo vya ukatili kwa asilimia 70


 

Na Asha Mwakyonde, Dodoma

WAZIRI  wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu,Dk.Dorothy Gwajima amesema ukatili wa majumbani ni sababu mojawapo inayowafanya watoto wakimbilie mitaani na matokeo yake wanakutana na aina zingine za ukatili na mazingira hatari zaidi.

Pia amesema takwimu zinaonesha waathirika wakubwa wa vitendo vya ukatili kwa upande wa watoto 70% ni wa kike pamoja na serikali na wadau wake kuendelea kupambana kuzuia ukatili huo.

Hayo ameyasema leo Januari 25,2022, jijini Dodoma katika ziara yake alipotembelea Makao ya kulelea Watoto yatima na Wazee wasiojiweza cha of Love and Joy yaliyopo kijini Hombolo, amesema serikali  inatoa huduma kwa wahanga wa ukatili ikiwemo huduma ya kisheria ambapo kwa mwaka 2020/21 mashauri 3889 yamepelekwa Mahakamani na 1,504 yametolewa hukumu na mengine kazi inaendelea.

Dk.Gwajima amesema mbali na  ukatili kwa watoto hata watu wazima wanafanyiwa ukatili ambapo wanawake wanatengeneza 96% ya wanaoathirika.

"Ukatili kwa mtu yeyote haukubaliki, hivyo serikali kwa kushirikiana na wadau wake wote itaendelea kuimarisha utekelezaji wa afua zenye kuhamasisha kuzuia na kushughulikia aina zote za ukatili ili kuhakikisha jamii ya kitanzania inafurahia haki ya kuishi," amesema.

Waziri huyo amefafanua kuwa  baadhi ya hatua zinazoendelea kutekelezwa ni pamoja na
Kuendelea kujenga uelewa kwa jamii ya Tanzania kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia ili jamii yenyewe iweze kuchukua hatua za kukataa na kuepuka mambo ya ukatili na pia jamii iweze kutoa taarifa pale wanapoona viashiria au vitendo vya ukatili.

Ameongeza kuwa hatua nyingine ni kuimarisha uratibu wa wadau wanaotekeleza afua za kuzuia na kushughulikia ukatili sambamba na kuimarisha mifumo ya utoaji wa taarifa za viashiria au matukio ya ukatili katika familia na jamii.

Pia ameleza kuwa hatua hizo ni pamoja na kuendeleza "TWENDE PAMOJA UKATILI SASA BASI" ili kila mdau kwa nafasi yake aweze kuelimisha jamii juu ya athari za vitendo vya ukatili na jinsi ya kuzuia ukatili, kuhamasisha uanzishaji wa vituo vya huduma za msaada wa kisaikolojia na kijamii ili kutoa huduma za ushauri na msaada kwa watu wenye msongo wa mawazo na matatizo mbalimbali ili waepuke kuingia kwenye mawazo ya kufanya ukatili.

Amesema, kuhamasisha uanzishaji wa vituo vya huduma kwa wahanga wa ukatili ikijumuisha nyumba salama na  vituo  vya mkono kwa mkono na kuwezesha upatikanaji wa wataalamu hususan wa kada ya ustawi wa jamii wenye upungufu mkubwa ngazi ili pamoja na majukumu mengine.

Pia ameongeza watashughulikia kwa ufanisi usuluhishi wa migogoro ya kijamii ikiwemo ya ndoa na familia kwa ushirikiano na viongozi wa kidini na kimila pamoja na  mabaraza ya Wazee.

Waziri Gwajima amesema pamoja na kuimarisha  Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto katika ngazi ya Taifa, Mkoa, Wilaya, Kata, Mitaa, Vijiji na Vitongoji kwa ajili ya kuzuia vitendo vya ukatili na kushughulikia matukio ya ukatili kama ilivyoelezwa kwenye Mpango Kazi wa Taifa wa Kupambana na Ukatili wa Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) 2017/18-2021/22.

"Wito wangu kwa jamii yote, TWENDE PAMOJA UKATILI SASA BASI tutoe taarifa za viashiria vya ukatili na ukatili wa aina zote kwenye mapambano dhidi ya aina zote za ukatili jamii yote inahusika, tuungane," amesema Waziri huyo.

Dk. Gwajima amebainisha kwamba serikali kwa kushirikiana na wadau wake inatekeleza kuhakikisha ustawi wa jamii kwa wazee waliotambuliwa kuwa hawajiwezi ambapo wameendelea kutunzwa kwenye makao 13 ya serikali ya wazee pamoja na makao mengine ya watu na taasis binafsi mfano wa Makao ya Hombolo.

Kwa mujibu wa waziri huyo mojawapo ya hitaji kubwa la wazee kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya CCM 2020-2025 ni pamoja na kuimarisha mabaraza ya wazee ngazi zote.

"Nipende kusema kuwa, taratibu za kuzindua rasmi baraza la kitaifa la wazee zimekamilika na matarajio ni Februari, 2022 uzinduzi ufanyike. Sera ya wazee inaendelea kufanyiwa kazi na iko kwenye hatua nzuri," anesema Dk. Gwajima.

Amesema masuala mengine yote yatokanayo na mapendekezo ya mabaraza yao yataendelea kufanyiwa kazi ili kuimarisha ustawi wa jamii kwa wazee.

Aidha amewashukuru kituo cha Home of Love and Joy kwa kuwapatia nafasi ya kubadilishana uzoefu na kwamba kazi yao ni njema kwani wamejifunza mengi.

Naye Naibu Waziri Mwanaidi Ali Khamis amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kuamka na kufanya kazi yao waliyokusudiwa katika kuhakikisha jamii inapata uelewa wa masuala ya ukatili na athari zake kwenye jamii.


No comments:

Post a Comment

Pages