January 13, 2022

Mwalimu Saidi: endapo nitapata Uspika nitaendesha Bunge kisayansi


Mwalimu Fikiri Saidi akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukubidhiwa fomu ya kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Na Asha Mwakyonde, Dodoma

ALIYEWAHI kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Fikiri Saidi leo amejitokeza kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hatua ya kuchukua fomu inatokana na nafasi hiyo kuwa wazi baada ya aliyekuwa Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Kongwa Job Ndugai kujiuzulu.

Akizungumza jijini Dodoma leo Januari 13, 2022 Saidi ambaye pia ni mwalimu na mjasiriamali kutoka katika Halmashauri ya Mwanza amejitokeza kuchukua fomu hiyo ya kugombea kiti cha Spika amesema kwa kuwa ni miongoni mwa Watanzania wenye haki ya kikatiba.

Saidi ambaye pia ni mwanafunzi wa PhD kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),amesema kuwa ameona masuala mengi hayaendi vizuri katika muhimili huo wa Bunge na kwamba endapo atapata nafasi kwa uzoefu wake kiutumishi wa Umma atahakikisha anaendesha Bunge hilo kwa ubora wa kipekee

Amesema ushiriki wake katika siasa ameweza kugundua masula mengi ya Watanzania ambayo yanapaswa kusimamiwa na Bunge hilo katika sheria na kanuni ambazo zinashindwa kukidhi matakwa ya Watanzania.

" Natosha kusimamia muhimili wa Bunge, msimamo wangu katika muhimili huu ni kama mingine ni kuzingatia na kuelewa kanuni na sheria," amesema Mwalimu Saidi.

Mwalimu Saidi mihimili mitatu inatekelezwa na sheria na kanuni za katiba ya nchi na kwamba msimamo wake utajikita kutokana na katiba hiyo inavyoelekeza.

Ameongeza kuwa matarajio yake endapo atapata nafasi hiyo Watanzania wategemee Bunge ambalo litafanya kazi kisayansi, kwa vitendo katika shughuli zake zote za kisheria na kanuy zake.

No comments:

Post a Comment

Pages