January 14, 2022

Prof.Lubua: Endapo nitapata nafasi wananchi wategemee Sera zilizochambuliwa

 


Mhadhiri  wa Chuo Cha Uhasibu kilichopo Arusha, Profesa Edison Lubua  akizungumza na waandishi wa habari  baada ya kutoka kuchukua ya kuwania nafasi ya Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Na Asha Mwakyonde, Dodoma

MHADHIRI wa chuo Cha Uhasibu kilichopo Arusha Profesa Edison Lubua  amechukua fomu ya kuwania nafasi ya Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivi karibuni aliyekuwa Spika wa Bunge hilo na Mbunge wa Jimbo la Kongwa Job Ndugai alijiuzulu nafasi hiyo na kuachwa wazi.

Prof. Lubua ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Mkoa wa Kilimanjaro, mjumbe kamati ya utekelezaji wazazi na ni Mjumbe wa mkutano mkuu ndani ya Chama Cha Mapindizi (CCM), mkoani humo amesema kuwa amechukua fomu kwa kuwa anaamini kila mmoja  anamchango wake ambao anapaswa kuutoa katika Taifa lake kwa nafasi aliyonayo.

Akizungumza na waandishi wa habari  mara baada ya kukabidhiwa fomu hiyo jijini Dodoma jana alisema kuwa elimu yake itamsaidia kuweza kuchambua masuala ya Sera ya nchi, bajeti na kuwaongoza wabunge kuzichambua Sera hizo.

Alisema kuwa kwa yale aliyopitia katika umri aliyonao  anaamini anauzoefu kupitia kufundisha watu mbalimbali wakiwamo watumishi wa Umma na hata wabunge pia.

"Pia katika uzoefu ambao nimekuwa nikiupata katika masuala ya ushauri, na uzoefu ndani ya Chama umenipatia nafasi kuweza kufahamu Chama pamoja na kulihamu  Taifa vizuri," alisema Prof. Lubua.

Alisema kuwa endapo atapata nafasi hiyo wananchi wategemee Sera zilizochambuliwa vizuri kitaalamu ambazo zinagusa maisha yao.
 

No comments:

Post a Comment

Pages