Na Lydia Lugakila, Bukoba
Wadau wa maendeleo katika kata ya Ruzinga Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera wamefanikiwa kufanya mambo mbalimbali ya kimaendeleo katika kata hiyo ikiwa ni pamoja na kubomoa jengo la shule ya msingi Ruhija ambalo lilikuwa limechakaa na kuonekana kuwa katika hali ya hatari kwa wanafunzi na walimu.
Hayo yamebainishwa na mwenyekiti wa sherehe ya ‘RUZINGA DAY’ Bi. Elizabeth Rugega wakati akisoma risala mbele ya mgeni rasmi ambapo amesema kuwa wadau wa maendeleo katika kata yao wamefanikiwa kufanya mambo mbalimbali ya kimaendeleo kwa nguvu zao huku ofisi ya mkurugenzi wa wilaya hiyo ikitoa ushirikiano mkubwa.
Wadau hao tayari wameanza ujenzi ambao unaendelea mpaka sasa ikiwa ni pamoja na kuweka umeme katika shule ya sekondari Ruzinga,kuchangia ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya hiyo, kununua vitanda kwa ajili ya kuwasaidia wanafuzi wa bweni pamoja na kukarabati wa madarasa yaliyoaribiwa na tetemeko.
Aidha,Bi Rugega amemuomba Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Misenyi Waziri Kombo kuwasaidia kumalizia ujenzi wa vyumba vya madarasa pamoja na nyumba ya walimu pindi ujenzi huo utakapofikia katika hatua ya rinta.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Ruzinga Rafiu Hussein amemshukuru mgeni rasmi kwa kuitikia wito wa kuungana nao katika siku ya ‘Ruzinga day’ na kumuomba kuwapatia maganga wa maabara katika kituo cha afya cha Ruzinga kinachopatikana katani humo.
“Tumejitahidi sisi kama wadau wa maendeleo tukanunua darubini katika maabara ya kituo chetu lakini chakushangaza mpaka sasa imepita miaka mitatu hatuna mtaalamu wa kutumia kifaa hiki jambo linalotuumiza sana, tunaomba ofisi yako iweze kulitazama suala hili” alisema Rafiu.
Kwaupande wake mgeni rasmi katika sherehe hiyo ambaye pia ni mkurugenzi wa wilaya ya Misenyi Waziri Kombo ameupongeza uongozi wa Ruzinga day pamoja na wadau wa maendeleo kwa kazi nzuri za kimaendeleo wanazozifanya na kuwaahidi kuwa ofisi yake na serikari kwa ujumla itakuwa bega kwa bega kuakikisha yote waliyoyaomba yanapatikana.
“ Niseme kuwa serikali inapenda wananchi wajitoe ili wakishafika hatua Fulani serikali iweke nguvu zake ikiwa ni pamoja na kumalizia miradi hiyo, binafsi naahidi fedha zitaletwa katika kata hii kwa ajili ya kumalizia nyumba ya walimu na pindi mtakapofikia katika hatua ya rinta” alisema Kombo.
Akitolea ufafanuzi juu ya suala la ukosefu wa mtaalamu wa kutumia darubini katika kituo cha afya cha Ruzinga Kombo amesema kuwa suala hilo atalifanyia kazi na kuomba viongozi wa kata hiyo kuandika barua kwa ajili ya rejea.
No comments:
Post a Comment