Watoa huduma za afya ngazi ya jamii wapewa vifaa vya kujikinga na Corona.
Na Hamida Ramadhani, Dodoma
KAIMU Mkurugenzi wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Ray Masumo ameishukuru Serikali ya Canada kupitia Shirika lake la Nutrition International kwa kuendelea kuiunga mkono serikali ya Tanzania katika vita dhidi ya UVIKO-19 na changamoto nyingine za Kilishe ambapo serikali hiyo imetoa jumla ya katoni 6000 za Barakoa na vitakasa mkono lita 6000 vyenye gharama ya shilingi milioni 57 kwa mikoa 17 ya Tanzania bara na Zanzibar.
Akizungumza leo wakati wa makabidhiano hayo ya vifaa hivi hivyo kwa wawakilishi kutoka Ofsi ya Rais Tamisemi na Ofisi ya Rais Muungano na Mazingira Dkt Masumo amesema vifaa hivyo vitawasaidia watoa huduma ya afya waliopo mstari wa mbele katika kutoa huduma za afya ikiwemo Huduma ya mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto kwani malengo yaliyopo ni kuhakikisha ifikapo Mwaka 2025 watoto wote nchini wamefikiwa na huduma ya matone ya Vitamini A kupitia vituo vya afya vilivyopo nchini.
Amesema vifaa hivyo vya kujikinga na UVIKO-19 vilivyotolewa na tasisi ya Chakula na lishe Tanzania kupitia shirika la kimataifa ya Nutrition International (NI) vinakwenda kuwakinga watoa huduma ya afya wakati wa kampeni ya utoaji wa huduma ya Matone ya Vitamini A nchini hasa kwa Watoto.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Dkt,Aifello Sichalwe ambaye ndio aliyekuwa mgeni Rasmi kwa niaba ya Waziri wa Afya Dkt Dorothy Gwajima amesema vifaa hivyo vitakwenda kuwasaidia watoa huduma za afya walio mstari wa mbele katika kutoa huduma za afya nchini bila kuwasahau watoa huduma za afya ngazi ya jamii (CHW).
Dkt. Sichalwe amesema kutokana na changamoto ya UVIKO-19, Serikali inaendelea kuwapatia vifaa vya kujikinga na maambukizi ya UVIKO-19 watoa huduma waliopo katika vituo vya afya ili kuwawezesha kuendelea kutoa huduma za afya kwa ufanisi ikiwemo Kampeni ya utoaji wa Matone ya Vitamini A inayofahamika kama "Huduma ya Mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto".
“Vifaa hivi vimeanza kutolewa katika mikoa 12 ambayo ni Dodoma, Geita, Kagera, Morogoro, Katavi, Mwanza, Kilimanjaro, Shinyanga, Simiyu, Singida, Tabora na Tanga pamoja na Mikoa yote mitano ya Tanzania Visiwani. Ameongeza kuwa mikoa hiyo imechaguliwa kwa sababu ilikuwa na ufanisi duni katika utoaji wa hudumaza afya, hivyo kupitia msaada huu utasaidia kuimarisha kiwango cha ufanisi katika utoaji wa huduma za matone ya Vitamini A kwa watoto wengi zaidi” Alisema Dkt.Sichalwe.
Nae Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Nutrition International Dkt. Daniel Nyagawa amesema wamechukua uamuzi wa kutoa vifaa kwa Serikali ikiwa kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazochukuliwa katika kupambana na UVIKO-19 na wataendelea kushirikiana na afua nyingine ikiwemo zile za Kilishe ambazo shirika hilo limekuwa likizitekeleza hapa nchini.

No comments:
Post a Comment