Katibu mkuu wizara ya mifugo na uvuvi Tixon Nzunda, akiangalia monja ya chanjo zinazozalishwa katika Taasisi ya chanjo Tanzania Tv Kibaha.
Katibu Mkuu Nzunda akipata maelezo kutoka kwa Mtendaji Mkuu Tvl Dkt. Stella Bitanyi, juu ya ubora wa Chanjo zinazozalishwa na Taasisi yake.
Na Mwandishi Wetu
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw.Tixon Nzunda ameielekeza wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA) kufanya kazi Kibiashara ili iweze kujiendesha yenyewe bila kutegemea ruzuku kutoka Serikalini.
Nzunda ameyasema hayo jana (26/01/2022) alipofanya ziara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo Januari 08, 2022.
"Fanyeni kazi kibiashara na kwa uadilifu mkubwa ,mashamba ya mifugo yanayovamiwa na Wananchi hakikisheni mnayatumia kibiashara kwa kutenga fedha kwenye bajeti yenu ili yaweze kupimwa ili kuondokana na adha ya kuvamiwa na wananchi". Alisema Nzunda.
Mbali na suala la kuimarisha mashamba ya mifugo, Nzunda ameelekeza mifumo ya utendaji kazi ya Kielekroniki iimarishwe katika vituo vyote vya Wakala hiyo.
Akielezea kuhusu changamoto ya Uhaba wa Watumishi wa wakala hiyo, Nzunda amemuelekeza Mtendaji mkuu wa Wakala hiyo kufuatilia maombi ya kuajiri watumishi wapya Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma ili kukidhi mahitaji ya taasisi hiyo.
Vile vile Nzunda ameelekeza kulindwa na kutunzwa kwa Mali za wakala hiyo ili ziweze kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Pia, ameelekeza Wakala kufanya kazi kwa karibu na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini (GCU) cha Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kutangaza kazi nzuri zinazofanywa na wakala hiyo.
Aidha, Nzunda ameielekeza Wakala hiyo kukutana na wadau wanaotumia chanjo hizo kila mwaka ili kupata mrejesho kutoka wadau hao.
Nzunda alihitimish maelekezo yake kwa kuitaka wakala ijikite katika kutafuta masoko ya chanjo hizo nje na ndani ya nchi.
Awali akisoma taarifa fupi ya Wakala hiyo Mtendaji Mkuu wa Wakala hiyo Dkt. Stela Bitanyi alibainisha kuwa, kazi kubwa wanayofanya ni uchunguzi na utambuzi wa Magonjwa ya Wanyama na Wadudu wanaosambaza magojwa na uhakiki wa usalama na Ubora wa Vyakula vya Mifugo.
Pia Dkt.Stela amesema kuwa wakala inatimiza Majukumu yake kwa kupima,kutathimini na kuhakiki Vitendanishi, mimea tiba pamoja na kemikali zinazotumika katika maabara za Wanyama.
Dkt. Bitanyi aliongeza kuwa wakala hiyo kupitia Taasisi ya Chanjo nchini (TVI) inatengeneza na kuzalisha aina saba (7) chanjo dhidi ya magonjwa ya Mifugo ikiwa ni pamoja vitendanishi.
"Chanjo za Mifugo zinazozalishwa na TVLA ni pamoja naTemevac,(chanjo dhidi ya Mdondo), Kimeta, Chambavu,Tecoblax (Mchanganyiko wa Kimeta na Chambavu), Kutupa Mimba (Brucellosis), Homa ya Mapafu ya ng'ombe (CBPP) na Homa ya Mapafu ya Mbuzi (CCPP)" Amesema Dkt. Bitanyi.
Dkt. Bitanyi amebainisha kuwa ili kusogeza huduma karibu kwa wafugaji, vituo hivyo vya uchunguzi wa Magonjwa ya Mifugo vipo pia katika mikoa ya Arusha, Dodoma, Iringa, Mtwara, Mwanza, Sumbawanga, Tabora na Kliniki ya Mifugo na Maabara meatu-Simiyu.
Katika ziara hiyo Nzunda pia alipata fursa ya kutembelea kiwanda cha kuzalisha Chanjo kibaha (TVI) na kujionea jinsi chanjo za mifugo zinavyotengenezwa ambapo aliwataka wanasayansi hao kuongeza umahili na Weledi katika kazi zao na kuzingatia Uadilifu.
No comments:
Post a Comment