HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 26, 2022

WANANCHI JITOKEZENI KWA WINGI SENSA YA MWAKA 2022

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Balozi. Dkt.  Pindi Chana akizungumza katika kikao chake na Ofisi ya Taifa ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar kuhusu maandalizi ya Sensa  ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 katika Ukumbi wa Ofisi hiyo Jijini Dodoma  Januari 24, 2022.


NA MWANDISHI WETU


WANANCHI wamehimizwa kujitokeza wa wingi kushiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka 2022 nchi nzima kwa lengo la kupata takwimu sahihi kwa maendeleo ya Taifa  kwa ujumla.

 

Hayo yalisemwa Januari 24, 2022 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Balozi. Dkt   Pindi Chana alipofanya kikao na Ofisi ya Taifa ya Mtakwimu na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu maandalizi ya sensa ya watu na makazi Jijini Dodoma.

 

Mhe. Waziri Pindi alisema kuna umuhimu mkubwa wa kufanya sensa hiyo kwani itatoa takwimu muhimu ambazo Serikali itazitumia kufahamu mahitaji ya wananchi wake na miundombinu inayotakiwa kuboreshwa ili wananchi kupata huduma muhimu.

 

“Takwimu hizi  tunaweza kuzitumia kwa maendeleo yetu wenyewe kuna masuala ya  ujenzi wa  vituo vya afya, madarasa, uwekezaji wa aina mabalimbali na hata uchumi wa mtu mmoja mmoja unahitaji kujua idadi ya watu na makazi wakati umefika sasa tuendele kuhamasishana na kuelekezana kufafanua masuala haya ya sensa,” alisema Mhe. Dkt.Pindi.

 

Pia aliagiza Kamati za Sensa za Mikoa, Wilaya, Kata na Vitongoji kuundwa na kukutana kujadili masuala mbalimbali kuhusu maadalizi ya utekelezaji ya sensa hiyo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa manufaa ya wananchi.

 

“Kamati hizi ziwe zimeshaundwa na kukutana kuandaa maamdalizi ya utekelezaji wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 nalo ni jambo la msingi na wajumbe wa kamati za sensa nao wakutane waanze kutafakari masuala ya maandalizi na namna shughuli itakavyofanyika,” alieleza Mhe. Dkt.Pindi.

 

Hata hivyo alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu kufanyika kwa sensa mwaka huu na maandalizi ya serikali ya kuwezesha bajeti ya masuala ya sensa huku akiishukuru Serikali ya Zanzibar kwa ushrikiano mkubwa inyoonesha kuhakikisha sensa inafanyika kwa ustawi wa Nchi.

 

Naye Kamisaa  wa Sensa ya Watu na Makazi Zanzibar, Balozi Mohamed Haji Hamza alibainisha kwamba sensa hiyo itashirikisha makundi yote wakiwemo vijana, watu mashuhuri , nyumba za ibada  na viongozi wa kisiasa kufikisha ujumbe uliokusudiwa na kuhakikisha kila mwananchi anashiriki sensa.

 

“Tutaendelea kuhamasisha wananchi kushiriki katika sensa tutatumia makundi yote makanisani, misikitini, wapo wasanii, wastaafu na kila yakapofanyika maadhimisho ya kitaifa nia yetu wananchi wapate  taarifa ya sensa na umuhimu wake na mashirika ya umma pamoja na  maeneo yeyote yenye mkusanyiko wa watu na vyombo vya usafiri,” alifafanua Balozi Hamza.

 

Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa alieleza kwamba  sensa ya mwaka huu itafanyika kidigitali kupata taarifa sahihi na kwa wakati  kulingana na madodoso yanavyoelekeza ambapo tayari sensa ya majaribio imefanyika na elimu kuhusu sensa imetolewa kwa makarani wa sensa kuwajengea uwezo wa kukusanya taarifa kama inavyotakiwa.

 

“Makarani watakaokusanya taarifa hizi za makazi, majengo na watu tunawapa elimu namna ya kuuliza maswali kulingana na hali ya mtu aliyonayo hasa wenye ulemavu na sensa ya majaribo tuliyofanya imetupa mwanga mkubwa wa kile tunachoenda kukifanya na sensa hii itagusa hadi ngazi za vitongoji,” alisema Dkt. Albina.

 

Aidha akiwasilisha taarifa ya Maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 Mratibu wa Sensa kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Seif Kuchengo alieleza kwamba hadi sasa baadhi ya maeneo yametengwa  kwa ajili ya kufanyia sensa kwa Tanzania Bara  na Zanzibar.

 

“Kwa hali ya maandalizi ya sensa yanaenda vizuri kwani mwaka huu tutatumia vishikwambi katika ukusanyaji wa taarifa tofauti na awamu iliyoota na upande wa maeneo tumeshatenga  Tanzania Bara vitongoji 54, 989 kati ya vitongozi 64,318 sawa na asilimia 85 wakati mijini  imetengwa mitaa 1,984 kati ya 4, 281 wakati Zanzibar 3,497 katika Shehia 382 kati ya Shehia 388,” alisema  Mratibu huyo.
 

No comments:

Post a Comment

Pages