RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Dk. Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi Cheti cha Uzinduzi wa Jukwaa la Wahariri Zanzibar (TEF) Bw. Haji Suweid Ramadhan baada ya kumalizika kwa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa (TEF) uliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Unguja Jijini Zanzibar.
Zanzibar inathamini na kuhitaji sana mchango wa vyombo vya habari katika kufanikisha utekelezaji wa mipango yake mikuu ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa uchumi wa kisasa unaotilia mkazo matumizi ya rasilimali za bahari.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi aliyasema hayo leo huko katika ukumbi wa Idrissa Abdul Wakil, Kikwajuni Zanzibar wakati akiufungua Mkutano Mkuu wa Sita wa Jukwaa la Wahariri Tanzania kwa mwaka huu wa 2022.
Alisema kuwa Jukwaa la Wahariri Tanzania ni fursa muhimu kwa wanahabari kufahamu wajibu wao wa kubeba ajenda muhimu za maendeleo na kuwafikishia wananchi kwa lugha nyepesi na mbinu mbali mbali ili wahamasike kutumia fursa zilizopo katika Uchumi wa Buluu na kuyafikia malengo ya Serikali.
Hivyo, Rais Dk. Mwinyi aliwanasihi Wahariri, Waandishi wa Habari na wamiliki wa vyombo vya habari kutumia jukwaa hilo kujifunza na kuielewa kwa kina mipango mikuu ya Uchumi na kutoa ushauri wao pamoja na namna bora ya kuitekeleza.
Aliongeza kuwa bado zipo baadhi ya sheria ambazo huwenda zikawa kikwazo cha kuyafikia matarajio ya kuleta ustawi wa kiuchumi na kijamii hivyo ni dhahiri kuwa sheria ambazo ni kikwazo zinahitaji kufanyiwa mabadiliko na kurekebishwa ili ziendane na mwelekeo wa uchumi unaojengwa kwa kuzingatia maslahi ya nchi.
Rais Dk. Mwinyi alizielekeza taasisi zinazosimamia sheria pamoja na wadau wa sekta ya habari kwa kushirikiana na Tume ya Marekebisho ya Sheria Zanzibar kukaa pamoja na kuona namna bora ya kufanya marekebisho ili kuwa na Sheria ambayo itaweza kuzingatia wakati uliopo.
Aliwaahidi Wahariri kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya habari kwa kutambua na kuthamini mchango wake muhimu kwa maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii.
Kadhalika, Rais Dk. Mwinyi alieleza hatua zitakazochukuliwa katika kuviimarisha vyombo vya habari vya Serikali kwa namna mbali mbali ili navyo viweze kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya sekta ya habari na mawasiliano duniani na kuviwezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Rais Dk. Mwinyi alichukua fursa hiyo kutoa shukurani zake za dhati kwa Wahariri, Waandishi wa Habari na Wamiliki wote wa vyombo vya ahabri kwa ushiriki wao katika mikutano yake ya kila mwisho wa mwezi ambayo tayari ameshaifanya mara mbili.
Hata hivyo, aliwataka viongozi wengine wenye dhamana kutoa ushirikiano kwa wanahabari pale wanapohitaji kupata ufafanuzi wa masuala mbali mbali kwani wananchi wanahaki ya kusikia na kufahamu masuala mbali mbali yanayohusu maisha yao ikiwemo utekelezaji wa shughuli za Serikali.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza haja kutumia lugha nyepesi kuwasilisha dhana nzima ya uchumi wa Buluu kwa wananchi ili waweze kuufahamu na kuufanyia kazi vizuri.
Nae Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita alieleza mashirikiano mazuri yaliopo kati ya uongozi wa Wizara yake pamoja na uongozi wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye kwa upande wake alitoa pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi kwa juhudi zake za kuiletaa maendeleo Zanzibar na kuahidi kumuunga mkono huku akieleza azma ya Wizara yake katika kuhakikisha Sheria husika inafika pazuri kabla ya Bunge la Bajeti.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania Deodatus Balile kwa upande wake alitoa pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi kwa kuwaunga mkono kwa kiasi kikubwa katika kufanikisha shughuli yao hiyo.
Alieleza azma ya Mkutano huo wenye kauli mbiu ya “Uchumi wa Buluu na Mawasiliano ya Umma” ambayo ina lengo la kumuunga mkono Rais Mwinyi katika dhana yake ya Uchumi wa Buluu ambao kwa mara ya kwanza tokea kuundwa kwa Jukwa hilo mnamo mwaka 2009 unafanyika hapa Zanzibar.
Pia, alisema kuwa kwa mara ya kwanza mkutano huo unawahusiha wajumbe kutoa nchi za Kenya, Malawi, Uganda, Zimbabwe, Rwanda na Burundi.
Katika mkutano huo mada mbili zilitolewa ambazo zote zimejikita na hali halisi ya uchumi wa Buluu ambapo watoaji mada walikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu Dk. Aboud Jumbe pamoja na Mwandishi mkongwe wa habari Salim Said Salim.
Katika mkutano huo pia, Rais Dk. Mwinyi alilizindua Jukwa la Wahariri la Zanzibar pamoja na kutoa vyeti kwa wafadhili waliofadhili mkutano huo.
No comments:
Post a Comment