HABARI MSETO (HEADER)


March 09, 2022

Prof. Mkenda: Rais Samia amewekeza sekta ya elimu, ufundi


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Machi 9, 2022 kuhusu mafanikio ya wizara hiyo katika Mwaka Mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Caroline Nombo.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, akizungumza na waandishi wa habari wakati akielezea mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita katika sekta ya elimu.

Baadhi ya wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu.

 

Na Mwandishi Wetu


WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuboresha vyuo vya ufundi ili kuongeza wigo wa vijana kujiajiri kwenye sekta ya ufundi.

Akizungumzia mafanikio ya mwaka mmoja wa utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan, Profesa Mkenda amesema dhamira hiyo imejidhihirisha kwa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Dodoma ulioanza Mei 28 mwaka 2021. 

Amesema hayo leo Machi 9,2022 alipozungumza na wanahabari kuhusu mafanikio ya sekta ya elimu kwa kipindi cha mwaka mmoja wa utawala wa Rais Samia na kumpongeza kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika katika wizara hiyo.

“Chuo hiki cha Dodoma kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 3,000 kwa mwaka mmoja wa masomo na kuongeza fursa za elimu ya ufundi kwa lengo la kuongeza nguvu kazi ya watu wenye ujuzi hapa nchini.

“...Tunatarajia ujenzi wa chuo hiki utakamilika katika kipindi cha miezi 18 kwa gharama ya Sh. bilioni 17.9 ambapo hadi Januari 2021, serikali imekwisha kutoa Sh. bilioni 3.92 za awali. Hadi sasa ujenzi umefikia kwa asilimia 45 na kitakamilika Desemba 30,2022,” amesema Profesa Mkenda.
 
Kuhusu Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA), Januari mwaka huu, Serikali imetoa Sh. bilioni 30.84 kwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (VETA) kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi vya Wilaya 25 hivyo kuongeza fursa za upatikanaji wa Elimu ya Ufundi. 

Amesema kati ya fedha hizo, Sh. bilioni 28.7 zimetolewa kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO 19 (TCRP).
 
Kwa mujibu wa Profesa Mkenda, ili kuhakikisha fursa za upatikanaji wa elimu ya ufundi inaongezeka, maeneo mengine ya mafanikio katika uimarishaji wa Eimu hiyo ni kuendeleza ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi katika Mikoa ambayo ilikuwa haina vyuo hivyo.

Ameitaja mikoa hiyo kuwa ni Njombe, Rukwa, Geita na Simiyu ambapo Desemba,2021 Serikali imetenga Sh.16,830,582,822.31 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo hivyo ulioanza Januari 2022.

Amesema utoaji wa mafunzo ya Ufundi Stadi kwa Makundi Maalumu ya Vijana, ambapo vijana 8,000 wa kitanzania watanufaika ambapo Serikali imetoa Sh. bilioni 1.81 ili kuwawezesha kujengewa ujuzi na hivyo kujiajiri na kuajiriwa.

*Mitaala*
Waziri Profesa Mkenda amesema wataalam wa elimu na sekta mbalimbali wapo kwenye mchakato wa kuboresha mtaala wa elimu ili kuondoa ukakasi uliopo kwenye mtaala huo.

Amesema baada ya mapitio ya sera ya elimu ya mwaka 2014 amebaini uwepo wa mambo mazuri kwenye sera hiyo huku akishangazwa na kutotekelezwa kwa baadhi ya mambo.

“Elimu ya lazima ni miaka 10 lakini haikutekelezwa vitu kama hivi ni vizuri unashindwa kujua vimekwamia wapi,” amesema Profesa Mkenda.

Amebainisha kwamba ni azma ya Rais Samia kufumua sekta ya elimu na kuona mageuzi kwenye sekta hiyo kuanzia eneo la mtaala.

“Kazi hiyo inaendelea wataalam wamejifungia wanapitia kipengele kwa kipengele... tutakuwa na kongamano kubwa la elimu hivi karibuni ambapo wadau kutoka ndani na nje ya nchi watashiriki. Yatafanyika makongamano mengine ili tupate mtaala bora wa elimu,” amesema waziri huyo.

*Elimu Maalum*
Katika kuboresha utoaji wa elimu maalum na kuongeza nafasi za mafunzo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, Serikali inakamilisha ujenzi wa shule jumuishi ya mfano ya Lukuledi iliyopo Masasi Mkoani Mtwara itakayokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 620. 

Serikali imewezesha uchapaji wa vitabu vya wanafunzi wenye mahitaji maalum katika ngazi ya Sekondari ambapo jumla ya vitabu 9,178 kwa wanafunzi 353 wasioona na vitabu 93,366 kwa ajili ya wanafunzi 3,591 wenye uoni hafifu wa elimu ya sekondari kwa thamani ya Sh 707,000,000. 

Vilevile, Serikali imewezesha ununuzi wa vifaa saidizi kwa wanafunzi 486 wenye mahitaji maalum wa Elimu ya Juu katika taasisi 11 za umma vyenye thamani ya Sh. 770,000,000.
 
Mwaka wa fedha 2021/22, Serikali imenunua vishikwambi (Tablets) 330 vyenye gharama ya Sh. milioni 134 kwa ajili ya shule 15 za msingi zinazopokea wanafunzi viziwI. 

Amesema serikali pia imenunua vitimwendo 1,334 vyenye thamani ya Sh.milioni 191 kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa viungo waliobainika kuwa na uhitaji katika shule za msingi na sekondari.

No comments:

Post a Comment

Pages