Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Abdulrahman Kinana akizungumza na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dk. Donald J. Wright (kushoto) leo katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar Es Salaam. (Picha na Fahad Siraji).
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM-Bara), Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana, amekutana na Balozi wa Marekani nchini, Donald Wright, jijini Dar es Salaam ambapo wamezungumza mambo mbalimbali ikiwemo kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na nchi ya Marekani.
Akizungumza muda mfupi baada ya balozi huyo kuondoka Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam, leo Aprili 11 2022, Kanali Mstaafu Kinana alisema mazungumzo hayo yalikuwa ya kawaida katika kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na nchi hiyo.
“Mazungumzo yetu yalikuwa ya kawaida, tumezungumzia namna ya kuimarisha uhusiano pamoja na ustawi wa wananchi,” alisema Kanali Kinana.
Alisema miongoni mwa maeneo waliyoyagusia katika mazungumzo yao ni pamoja na kuimarisha huduma za kijamii ikiwamo afya na utoaji haki kupitia mifumo mbalimbali.
Viongozi hao wamekutana zikiwa siku chache tangu balozi huyo alipokutana na Rais Samia Suluhu Hassan.
No comments:
Post a Comment