Dar es Salaam – Tanzania inapoadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa kwa Mwalimu Julius Nyerere wiki hii, Ubalozi wa Marekani umeadhimisha siku hiyo kwa kufadhili maonyesho ya kihistoria katika Makumbusho ya Taifa na Nyumba ya Utamaduni yakiangazia urafiki kati ya Nyerere na Rais wa 35 wa Marekani, John F. Kennedy.
Maonyesho hayo yamezinduliwa leo asubuhi katika hafla fupi iliyohuduriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho, Dk. Noel Lwoga na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dr. Donald Wright.
Maonyesho haya yaliyopewa jina: “Julius Nyerere na John F. Kennedy: Urafiki Uliojenga Historia,” yanaonyesha picha, nyaraka na barua mbalimbali kati ya viongozi hawa wawili. Aidha, yanaonyesha jinsi viongozi hawa wawili walivyovutiwa na kila mmoja wao, jambo lililojidhihirisha katika uhusiano imara kati ya Marekani ni Tanzania, uhusiano ambao umedumu kwa zaidi ya miaka sitini.
“Urafiki kati ya viongozi hawa wawili ulikuwa msingi wa urafiki baina ya mataifa na watu wa nchi hizi mbili, urafiki ambao umeweza kudumu kwa muda mrefu,” alisema Balozi Wright katika hotuba yake.
Balozi Wright alitumia fursa hiyo kuenzi maisha na urithi wa Mwalimu Nyerere, ambaye kama angelikuwa hao, mwaka huu angekuwa anatimiza umri wa miaka 100.
“Naungana na Watanzania wote na watu wengine duniani kote kuenzi uongozi wa Nyerere katika kipindi chote cha maisha yake akitumikia umma: Akiwa muumini kijana wa uhuru kutoka ukoloni; akiwa baba wa taifa la Tanzania na rais wa kwanza wa nchi hiyo kwa zaidi ya miaka miwili kabla ya kung’atuka kwa hiari; akiwa ni msukumo kwa nchi kuingia katika zama mpya ya demokrasia ya vyama vingi na uchumi huria; na akiwa mzee mzalendo na mtetezi wa amani na usalama katika kanda,” alisema.
Maonyesho haya ni ya bure na wazi kwa wananchi wote.
No comments:
Post a Comment