April 25, 2022

MICHUANO YA KOMBE LA MEI MOSI TAIFA 2022

  Scolastica atwaa tena ubingwa  baiskeli 


Mchezaji Scolastica Hamis wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) akimaliza mbio za baiskeli za kilometa 15 kwa wanawake za mashindano ya Kombe la Mei Mosi Taifa zilizoanzia eneo la Chisichiiri na kumalizikia Isanga Plaza jijini Dodoma. Ushindi wa pili na tatu umekwenda kwa Bertha Mtanga wa TEMESA na Alavuya Mtalima wa Wizara ya Mambo ya Ndani.

 

 

Chaptelel Muhumba wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) ameibuka mshindi wa tatu wa mbio za kilometa 21 kwa wanaume zilizoanzia eneo la Matumburu na kumalizikia Isanga Plaza ikiwa ni moja ya michezo ya michuano ya kombe la Mei Mosi Taifa inayofanyika jijini Dodoma.

 

 Na Mwandishi Wetu, Dodoma

 

BINGWA mara tatu mfululizo wa michuano ya Kombe la Mei Mosi, Scolastica Hamis wa timu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), ametwaa tena ubingwa wa kuendesha baiskeli kwa upande wa wanawake baada ya kumaliza mbio za kilometa 15 zilizoanzia eneo la Chisichiiri na kumalizikia Isanga Plaza.

Scolastica, ni bingwa miaka mitatu mfululizo amesema amekuwa akitwaa ubingwa mara kwa mara katika michuano hii na ile ya Shirikisho la michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) kutokana na kuupenda mchezo huo na pia kufanya mazoezi kwa bidii akizingatia maelekezo ya makocha wake.

“Huu mchezo upo damuni mwangu yaani nahisi nisipocgeza ninaumwa ndio maana nimekuwa nikishiriki sana kwenye mashindano mbalimbali na ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu, Sekta yangu ya Uchukuzi na taasisi yangu Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kwa kunipa ushirikiano na msaada mkuibwa wa kushiriki kwenye michuano hii na mingine,” amesema.

Hatahivyo, ushindi wa pili kwa wanawake umechukuliwa na Bertha Mtanga wa TEMESA na ushindi wa tatu umekwenda kwa Alavuya Mtalima wa Wizara ya Mambo ya Ndani.

Kwa upande wa wanaume mchezaji Steven Sanga wa timu ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ametwaa ubingwa baada ya kuwabwaga wachezaji wakongwe na wazoefu katika mbio za kilometa 21 zilizoanzia eneo la Matumbura na kumalizikia Isanga Plaza.

Sanga amesema siri ya ushindi wake ni kumtanguliza Mungu mbele, pamoja na kufanya mazoezi kwa bidii kwa kuyafuata maelekezo ya makocha.

“Ninamshukuru sana sana Mungu kwa kutwaa ushindi wa kwanza maana mbio zetu zilikuwa na ushindani mkubwa sana, hivyo ninaahidi kuendelea kutwaa ubingwa katika michuano mingine ijayo,” amesema Sanga.

Wazoefu walioangukia pua na kushika nafasi ya pili ni Hassan Ligoneko wa Wizara ya Afya na aliyeshika nafasi ya tatu ni Chaptelel Muhumba wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi).

Mbio hizo zimeshirikisha wachezaji 18 kwa upande wa wanaume na 10 kwa upande wa wanawake.

Michuano hii ambayo inatarajia kufikia kilele tarehe 29 April, 2022, itaendelea leo kwa michezo ya jadi ya kucheza draft, bao na karata, itakayofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini hapa.   



.

 

 

No comments:

Post a Comment

Pages