April 14, 2022

MRADI WA MAJI WA BILIONI 69 UNATEKELEZWA MWANZA

 

Ninaiona Mwanza yenye maji ya kutosha ipo njiani- RC Mwanza


 

 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel akielekeza jambo wakati wa ziara yake kwenye ujenzi wa mradi wa chanzo kipya cha maji cha Butimba, Mkoani Mwanza.

 

Na Mohamed Saif

 

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel ameridhishwa na hatua za ujenzi wa mradi wa chanzo kipya cha maji katika eneo la Butimba wenye thamani ya shilingi bilioni 69 na utakaonufaisha zaidi ya wakazi 400,000.

Mhandisi Gabriel ameeleza hayo Aprili 12, 2022 wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi inayotekelezwa kwa fedha za Serikali Kuu ikiwemo mradi huo wa chanzo hicho kipya cha majisafi cha Butimba.

“Nimeridhishwa na shughuli inayoendelea hapa; ikumbukwe kwamba huu ni mradi wa kimkakati ambao Serikali imewekeza fedha nyingi ili kutatua adha ya upungufu wa upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wakazi wa Jiji la Mwanza,” alisema Mhandisi Gabriel.

Alisema anatambua uwepo wa mgawo wa huduma ya maji kutokana na hali halisi ya mahitaji ambayo ni makubwa kuliko uzalishaji wa maji wa sasa wa MWAUWASA; hata hivyo alibainisha jitihada mbalimbali za Serikali ya awamu ya sita inayooongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha huduma ya majisafi inaimarika zaidi.

“Tunamshukuru sana Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa dhamira yake ya dhati ya kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani, fedha za miradi zipo na zinafika kwa wakati na miradi inaendelezwa kwa kasi,” alisema Mhandisi Gabriel.

Mhandisi Gabriel alisema wananchi wamekuwa na hofu ya muendelezo wa ujenzi wa miradi na hivyo kupitia ziara yake hiyo kwenye mradi wa chanzo kipya cha maji eneo la Butimba anawathibitishia hatua za kimapinduzi zinazochukuliwa na Serikali ya awamu ya sita.

“Niwasihi wananchi waendelee kuwa na subira kwa niliyoyashuhudia hapa ninasema yajayo yanafurahisha. Mkandarasi nimemkuta site, kazi zinaendelea na mradi ni mkubwa ninawapongeza sana Wizara ya Maji kupitia MWAUWASA; ninaiona Mwanza yenye majisafi ya kutosha ni suala la muda tu, kazi inaendelea,” alisema Mhandisi Gabriel.

Akizungumzia utekelezwaji wa mradi, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele alisema mradi unatekelezwa na Mkandarasi Kampuni ya SOGEA SATOM na VINCI GRAND PROJETS kutoka Ufaransa.

“Shughuli za usanifu na ujenzi zilianza rasmi Februari, 2021 na tunatarajia ifikapo Februari 2023 mradi utakuwa umekamilika,” alibainisha Mhandisi Msenyele.

Mhandisi Msenyele alisema mradi unahusisha ujenzi wa chanzo kipya na kituo cha tiba ya maji chenye uwezo wa kusafisha na kuzalisha majisafi kiasi cha lita milioni 48 kwa siku.

“Chanzo hiki kitakapokamilika kitaboresha huduma ya upatikanaji wa majisafi kwa wakazi zaidi 400,000 katika jiji la Mwanza na maeneo ya pembezoni kama vile Usagara, Kisesa, Buhongwa Mashariki, Lwanhima, Sahwa, Fumagila, Kishiri, Igoma na Buswelu,” alisema Mhandisi Msenyele.

Mhandisi Msenyele alisema mradi unatekelezwa kwa mfumo wa kusanifu na kujenga na kwamba hadi kufikia Machi 2022, utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 90 kwa kazi ya usanifu na asilimia 12 kwa shughuli ya ujenzi.

 

No comments:

Post a Comment

Pages