April 14, 2022

TANZANIA KUWA NCHI YA KWANZA AFRIKA KWA KUSAMBAZA UMEME VIJIJINI


Mkuu wa Mkoa Singida Dk.Binilith Mahenge akishiriki kujenga Shule Mpya ya Sekondari inayojengwa Kitongoji cha Kisubio Iguguno wilayani Mkalama mkoani hapa wakati wa ziara yake kikazi ya siku moja ya kukagua baadhi ya miradi ya maendeleo inayoendelewa kutekelezwa  ya Sekta ya Afya, Maji na Elimu iliyofanyika jana.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Sophia Kizigo akishiriki kujenga Shule Mpya ya Sekondari inayojengwa Kitongoji cha Kisubio.

Mkuu wa Mkoa Singida Dk.Binilith Mahenge akisisitiza jambo wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wilaya hiyo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Sophia Kizigo.
Mkuu wa Mkoa Singida Dk.Binilith Mahenge akishiriki kuchimba msingi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Gumanga.


Na Dotto Mwaibale, Singida


MKUU wa Mkoa wa Singida Dk.Binilith Mahenge amesema Tanzania itakuwa nchi ya kwanza Barani Afrika  kwa kusambaza umeme katika vijiji vyote.

Dk. Mahenge ameyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Gumanga iliyopo Wilaya ya Mkalama katika ziara yake kikazi ya siku moja ya kukagua baadhi ya miradi ya maendeleo inayoendelewa kutekelezwa  ya Sekta ya Afya, Maji na Elimu.

Miradi aliyoitembelea na kuikagua ni ujenzi wa shule mpya ya Sekondari inayojengwa Kitongoji cha Kisubio katika Kata ya Iguguno ambapo ujenzi wake utagharimu Sh.600 Milioni, ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Gumanga Sh.500 Milioni ambapo wamepokea nusu yake Sh.250 Milioni na mradi wa maji uliopo katika Kijiji cha Milade ambao utagharimu Sh. 502 Milioni.

"Tumshukuru sana Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan huyu  mama ni wa mfano kwani ametoa fedha zaidi ya Sh. 60 Bilioni kwenye eneo la umeme amini usiamini Tanzania tutakuwa wa kwanza kwa kusambaza umeme vijiji vyote Barani Afrika ifikapo 2025" alisema Mahenge huku akishangiliwa.

Alisema katika wilaya hiyo vijiji vyote ambavyo havina umeme kuna mkandarasi yupo kazini akiweka miundombinu ya umeme ambao ukikamilika utatoa fursa kwa wananchi kuweka mashine za kusaga, saluni za kike na kiume na biashara zingine mbalimbali zinazotegemea umeme.

Alisema katika Mkoa wa Singida una vijiji 441 na kati ya hivyo 176 vilikuwa havina umeme lakini sasa vijiji vyote hivyo Rais Samia Suluhu Hassan anaweka umeme ili ni jambo kubwa la kujivunia ambalo halijawahi kutokea hapa nchini na kuwa tayari kuna wakandarasi wawili wanapiga kazi mmoja anahudumia katika Wilaya ya Iramba na Mkalama na mwingine anahudumia Wilaya ya Ikungi, Manyoni na Singida Vijijini.

Alisema katika Mkoa wa Singida Rais Samia ametoa zaidi ya Sh.232 Bilioni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kati ya fedha hizo Sh. 30 Bilioni zimeelekezwa kwenye eneo la elimu ambapo shule mpya 9 zinajengwa kwa wakati mmoja.

"Mbali ya ujenzi wa shule hizo kuna zahanati zinajengwa, vituo vya afya, barabara na hapa kwenu Mkalama tayari daraja kubwa la Msingi ambalo limegharimu Sh.10 Bilioni limejengwa ambalo litawaunganisha na Mkoa wa Simiyu na Meatu hivyo kutimiza hoja ya kuwaletea wananchi wa Mkoa wa Singida na Wilaya ya Mkalama maendeleo" alisema Dk. Mahenge.  

Diwani wa Kata ya Gumanga Tarafa ya Nduguti na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, James Mkwega ambaye kwa kiasi kikubwa ndiye aliyefanikisha upatikanaji wa ujenzi wa kituo hicho cha Afya alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa Sh.500 Milioni kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kata hiyo ambapo alimuomba mkuu wa mkoa kumfikishia shukurani hizo.

"Sisi Wana Gumanga hatuna cha kusema shida yetu kubwa ilikuwa ni kupata kituo cha Afya ambacho kitawapunguzia adha wanananchi hasa wakina mama ambayo walikuwa wakiipata kwa kutembea umbali mrefu wa kilometa 33 kufuata huduma hiyo Kituo cha  Afya cha Kinyambuli na mjini Mkalama" alisema Mkwega.

Alisema walikuwa na uhitaji mkubwa sana wa kituo hicho kwani kuna wananchi wa Kitongoji  cha Kitulamando wapo umbali wa kilometa 25  Kijiji cha Mgimba  na wa Kijiji cha Lutang'ombe Kinankamba ambao wapo kilometa 30 waliokuwa wakitembea umbali huo kufuata huduma ya afya katika Zahanati ya Gumanga.

Mkwega alisema kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho kutasaidia wananchi zaidi ya 18,000 kutoka katika maeneo hayo kupata huduma kwenye kituo hicho cha Afya cha Gumanga ambacho kitakuwa kikitoa huduma ya Uzazi,  Upasuaji na jengo la kufulia.

 Mkuu wa Wilaya ya Mkalama , Sophia Kizigo alisema katika wilaya hiyo watakuwa na vituo vya afya vitatu ambavyo amevitaja kuwa ni cha Mkalama, Ilunda na cha Gumanga ambacho fedha zake tayari zimepokelewa na ujenzi wake umeanza.

"Ili ni jambo kubwa alilolifanya Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwani katika kipindi chake cha uongozi cha mwaka mmoja katika wilaya yetu ya Mkalama anatujengea vituo viwili vya afya vitakavyokuwa na sifa ya upasuaji hakikika ni kazi kubwa aliyotufanyia tunakila sababu ya kumshukuru na kumpongeza" alisema Kizigo huku wananchi wakipiga makofi ya kumpongeza Mama Samia.

No comments:

Post a Comment

Pages