April 14, 2022

Wanahabari, TMA wajadili mabadiliko ya tabia nchi

Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi, Akizungumza na waandishi wa habari.

Maalam wa masuala ya hali hewa kutoka kituo cha utabiri na matumizi ya hali hewa (ICPAC), Dkt. Zewdu Segele akizungumzia utabiri wake wa Machi - Mei ambao iliutoa mwezi Februari.

 

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekutana na waandishi wa habari kujadili athari za mabadiliko ya tabia nchi katika mifumo ya hali ya hewa ikiwa ni maandalizi ya kurejea utabiri wa MASIKA uliotolewa Februari 2022. 

 

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi, amesema mifumo ya hali ya hali ya hewa imebadilika kutokana na mabadiliko ya tabia nchi yaliyopelekea kubadilika kwa mwenendo mzima wa mvua za msimu wa MASIKA 2022. Aliyazungumza hayo alipokuwa akifungua warsha ya wanahabari iliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya TMA, Ghorofa ya tatu, Ubungo Plaza, tarehe 12/04/2022.  

“Tanzania tumeanza kuziona athari za mabadiliko ya tabia nchi, katika mifumo ya hali ya hewa hasa kubadilika kwa joto la bahari ambalo kwa kawaida halibadiliki kwa haraka kutokana na tabia ya maji kutunza joto lake kwa muda mrefu.” Alisema Dkt. Kijazi.

Dkt. Kijazi alisema kuongezeka kwa joto duniani (global warming) kunasababisha kuyeyuka kwa barafu zilizoko katika ncha za dunia na hivyo kuongeza vina vya bahari katika maeneo mbalimbali duniani ikiwa Pamoja na kubadilika kwa hali ya joto la bahari na hivyo kuathiri mifumo ya hali ya hewa.

Aidha Dkt. Zewdu Segele ambaye ni mtaalam wa masuala ya hali hewa kutoka kituo cha utabiri na matumizi ya hali hewa (ICPAC) alisema, ICPAC imetoa mrejeo wa utabiri wake wa Machi – Mei ambao iliutoa mwezi Februari. Dkt. Zewdu alisema mifumo ya awali ilionyesha uwepo wa mvua za juu ya wastani katika nchi za pembe ya Afrika ikiwemo Tanzania, lakini baada ya mifumo kubadilika nchi hizo sasa zitapata mvua za chini ya wastani.

Dkt. Zewdu aliongeza kusema utabiri unaotolewa na ICPAC ni wa maeneo makubwa hivyo nchi wanachama wana jukumu la kuandaa utabiri wa maeneo madogo madogo katika nchi zao.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inatarajia kutoa rasmi mrejeo wa utabiri wa mvua za msimu wa Masika (MAM) 2022 Tarehe 13/04/2022.

No comments:

Post a Comment

Pages