Baadhi ya wabunifu wakisikiliza mada katika kongamano hilo.
Na Mwandishi Wetu
WIZARA ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki imesema itahakikisha inatoa ushirikiano kwa wabunifu waliopo nchini ili kuwawezesha kutangaza bunifu zao ndani na je ya Tanzania.
Hayo yamesemwa na Balozi Mindi Kasiga ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye Wiki ya Ubunifu Tanzania inayoendelea Ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam.
Wiki hiyo imeandaliwa na Wizara ya Elimu ,Sayansi na Teknelojia kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Sayansi ya Teknolojia (COSTECH) na UNDP kupitia Programu yake ya Funguo na Mdhamini Mkuu ni Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania.
Amesema wizara hiyo inataka kuona kunakuwa na wabunifu wengi zaidi ambao wanaibuliwa nchini kila siku na kwamba wabunifu wasikubali kuwa kimya badala yake wajitokeze na kwenda kutambuliwa na mamlaka husika.
“Niko hapa leo kwa ajili ya shughuli hii ya Wiki ya Ubunifu Tanzania inayoratibiwa na Ubalozi wa Uholanzi nchini Tanzania, kitu muhimu ambacho tumejifunza kutokana na mazungumzo tuliyoyafanya na wabunifu wa kitanzania kuna mambo ambayo yamejitokeza katika mazingira ya sasa hususani kwenye utali ambao ni lazima kuhusisha ubunifu.
“Hatuwezi kuendelea kutangaza utalii kwa njia zile zile za zamani ndio maana mpaka sasa hivi tunaona Rais wetu Mama Samia Saluhu Hassan akiendelea kufanya promosheni ya filamu ya Royal Tour inayoelezea vivutio vya utalii Tanzania kama nchi ya kipekee katika eneo la utalii,” amesema Balozi Kasiga.
Amesema hiyo Wiki ya Ubunifu Tanzania kupitia majadiliano yaliyofanyika leo wamejadili kwa kina nini kifanyike kwenye ubunifu kwa njia mbadala ya kutangaza na kuvutia watanzania kwenda kwenye utalii wa Tanzania.
“Kwa hiyo tulikuwa na mjadala tunaposema kutangaza utalii tunaanza na sisi wenyewe? Tunaanzaje au wanaanza wazungu? Tukaona yote yanahitajika na yote ni muhimu,” amesema Balozi Kasiga alipoelezea ubunifu katika kutangaza utalii.
Aidha katika majadiliano hayo wameangalia ni jinsi gani wanaweza kutumia teknolojia na ubunifu kama njia mojawapo ya kuleta maendeleo huku akitumia nafasi hiyo kumuelezea Mtanzania Idd John ambaye amekuja na ubunifu wa jukwaa la Safari Wallet.com.
“Jukwaa hilo unaweza kuingiza fedha kutoka kwenye simu yako ya kiganjani na ukaenda kutalii sehemu yoyote Tanzania kwa kutumia Wallet Safari kwanza unaweza kulipa fedha na kwenda kutalii kokote hapa nchini.
“Hivyo ni wajibu wetu Wizaara ya Mambo ya Nje na watanzania wengine kuangalia tunafanya nini kumsaidia Idd aliyebuni Wallet Safari, sisi kwa nafasi yetu tunasema tutampa kila aina ya ushirikiano na ndio wajibu wetu kumsadia kila mtanzania kwa kutumia balozi zetu tutamsaidia kutangaza jukwaa hilo,” ameseme.
Kwa mujibu wa Balozi Kasiga, wizara hiyo ni kiungo kiunganishi nchi za nje ambapo kuna wawakilishi (mabalozi) na wakati huohuo mataifa mengine nayo yanawawakilishi wao hapa nchini.
Kwa upande mwingine, mtoa mada katika majadiliano yaliyohusisha wabunifu na masuala ya kikodi Donald Nsanyiwa ambaye ni Mkurugenzi wa Kodi wa Kampuni ya KPMG, amesema jambo la msingi linalopaswa kuzingatiwa ni kufahamu masuala ya kodi.
“Tumejaribu kuwalezea wabunifu wakiwemo wanaojihusisha na ujasiriamali kuwa wanapowaona maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wanakuja kwenye biashara zao wasione kama wanawaingilia bali ni jukumu hivyo wanatakiwa kuwapa elimu ya kujua umuhimu wa kodi pindi wanapoanza biashara,” amesema.
No comments:
Post a Comment