May 11, 2022

TIRA yazipiga faini Kampuni Nne za Bima, yazitaka kulipa fidia


Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam 

Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima nchini (TIRA) imezipiga faini Kampuni nne za bima kwa kukiuka kanuni, taratibu na sheria zinazoongoza uendeshaji wa huduma za bima.

Kampuni zilizopigwa faini ni Insurance Group of Tanzania (IGT), Jubilee Insurance, Kampuni ya Resolution pamoja na  Kampuni ya UAP.

Akizungumza na wanahabari jijini humo Kamishna wa Bima Nchini, Dkt. Baghayo Sagware amesema kampuni zimepigwa faini kutokana na kukiuka taratibu na sheria ulipaji fidia kwa wateja pale wanapopata majanga.

" TIRA ina jukumu la kusimamia shughuli za bima, kutoa ushauri kwa Serikali hivyo leo tunasikitika kutoa taarifa ya mwenendo usiofaa wa kampuni nne za bima," amesema Dkt. Saqware.

Amebainisha kuwa TIRA Oktoba Mosi mwaka jana na Februari 15 mwaka huu ilipkea malalmiko 48 kutoka kwa wateja wa Kampuni ya IGT na kwamba walibaini ukiukaji wa sheria na taratibu za uendeshaji wa shughuli za bima ikiwemo kifungu namba 166 (1) cha sheria ya bima nchini.

Kamishna Saqware amesema kufuatia ukiukwaji huo kampuni hiyo imepigwa faini ya Sh Millioni 20 ambapo Mwenyekiti wa Bodi, Afisa Mtendaji Mkuu, Afisa Fedha Mkuu pamoja na Meneja wa Madai na Fidia kila mmoja wakitakiwa Sh Mil 5. 

Amesisitiza kuwa Kampuni ya Jubilee Insurance imepigwa faini ya Sh Mil 5 ambayo imeshlipwa  ikiamuru kampuni hiyo kulipa fidia ya Euro mill 511 kama inavyodaiwa na Wizara ya Maji baada ya kampuni ya ukandarasi ya Spencon kushindwa kutimiza wajibu wake wa kimkataba wa miradi ya maji wenye mkataba namba ME-011/2011-2012/W/O5 kwa Mamlaka ya Maji ya Mji wa Kigoma ambao ulikua umepewa Kinga na kampuni ya hiyo.

Ameongeza kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Jubilee Insurance amepigwa faini ya Sh Mil 10 kwa kutofuata sheria na taratibu za bima hivyo kuchafua taswira ya soko la bima nchini.

Kamishna Dkt. Saqware amefafanua kuwa Kampuni ya Resolution imepigwa faini baada kubainika kuwa na mwenendo mbaya wa uendeshaji hivyo Afisa Mtendaji Mkuu anatakiwa kulipa Sh Mil 5  na kwamba TIRA imeiwekea zuio la kuendelea kufanya biashara na matangazo ya bima kuanzia leo na kuitaka kuendelea kulipa madai yote yaliyopo na yatayokuja kuepuka kufutiwa leseni ya biashara.

Pia amesema Kampumi ya UAP imepigwa faini ya Sh Mil 30 kwa makosa mbalimbali ikiwemo kushindwa kushughulikia malalamiko ya wateja kwa haraka hivyo imeagizwa kulipa fidia ndani ya siku 7.

Aidha, Mamlaka hiyo imetoa onyo kwa kampuni za bima kuacha tabia ya kutoshughulikia wateja wanapowasilisha malalamiko yao zitakazobainika zitachukuliwa hatua kali za kisheria.

Wakati huo huo, TIRA imewaasa Watanzania kuendelea kutumia huduma za bima na kuwasilisha malalamiko yao kwa Kamishna wa Bima wanapoona hawatendewi haki na kampuni za bima.

Kwa upande wake, Meneja Utekelezaji Sheria na Kushughulikia Malalamiko wa TIRA, Jailo Mgavilenzi amesema kuwa Kampuni ya Jubilee ilikwenda kinyume cha sheria za Bima kwa kumlipa fidia dalali badala ya benki waliyokuwa wakiituma wateja kupata huduma za bima.



No comments:

Post a Comment

Pages