HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 02, 2022

Bilioni 6/- kufikisha maji kwa wananchi 80,000 Tanga


Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga, Mhandisi Pendo Omary akielezea waandishi wa habari namna fedha za ustawi zinavyotekeleza miradi ya maji mkoani humo.

 

Selemani Msuya, Tanga

 

WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mkoa wa Tanga umepanga kutumia Sh. bilioni 6.7 za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 kuwafikishia  maji safi na salama wananchi 80,000.

Fedha hizo ni sehemu ya mkopo usio na riba wa Sh.trilioni 1.3 za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), ambazo zimetolewa na Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya maji.

Hayo yamesemwa na Meneja wa RUWASA, Mkoa wa Tanga, Mhandisi Pendo Omary wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na wakala huo.

Mhandisi Omary amesema RUWASA Tanga imepokea Sh.bilioni 6.7 ambapo vijijini wamepeleka zaidi ya Sh.bilioni 5 zinazoteleleza miradi tisa na kunufaisha vijiji 21 na mijini zaidi ya Sh.bilioni 2 ambazo zinatumika kwenye miradi mitatu ya majimbo ya mjini.

“Fedha za ustawi hapa Tanga ni Sh.bilioni 6.7, ambazo zaidi Sh.bilioni 5 zinatekeleza miradi tisa kwenye vijiji 21 vya majimbo ya Kilindi, Pangani, Mkinga, Handeni Vijiji, Lushoto, Korogwe Vijiji, Mlalo na Bumbuli na zaidi ya Sh.bilioni 2 zinatekeleeza miradi mitatu ya mijini ambayo ni Tanga Jiji, Korogwe Mjini na Handeni Mjini,” amesema Mhandisi Omary.

Meneja huyo alisema katika Jimbo la Kilindi mradi unatekelezwa kijiji cha Lwande na Sagasi, Pangani Mikinguni na Stahabu, Korogwe kijiji Mgwashi Kwejibomi, Mkinga upanuzi wa Mradi wa Maji Parungu Kasela na Muheza Mradi wa Maji Mizembwe.

Mhandisi Omary amesema Handeni wanafanya upanuzi mradi wa maji uliopo na  Lushoto wanatekeleza miradi mitatu ambayo ni kuboresha miundombinu ya maji, mradi wa Mayo, Bungoyi na Kwesimu.

Amesema miradi hiyo ikikamilika itaongeza watumiaji wa maji safi na salama wapya 80,000 na kuufanya Mkoa wa Tanga kuongeza asilimia mbili ya upatikanaji wa maji, hivyo kuufanya mkoa huo kupata maji kwa asimilia 66 kutoka asilimia 64.

“Miradi hii tunatarajia ifikapo mwisho wa mwezi Mei maji yatakuwa yanatoka kila mahali, tunaomba wananchi watunze miradi hii, ili iwe endelevu,” amesema.

Mhandisi huyo amesema RUWASA wanamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kuwapatia fedha za miradi ya maji na kuahidi kuwa hawatamuangusha.

Omary amesema miradi ya maji ambayo inatekelezwa mkoa wa Tanga itawezesha kuongeza kasi ya uzalishaji na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Meneja huyo amesema pamoja na miradi hiyo ya ustawi, pia Tanga inatekeleza miradi mingine zaidi ya 18 ambayo kwa pamoja ikikamilika lengo la Serikali kufikia upatikanaji wa maji kwa asilimia 85 vijijini na 95 mijini litatimia.

No comments:

Post a Comment

Pages