May 27, 2022

DC IKUNGI AONGOZA UTATUZI WA MGOGORO YA ARDHI KATA YA PUMA NA DUNG'UNYI



Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Jerry Muro (kulia), akizungumza na wananchi wakati wa utatuzi wa mgogoro wa Ardhi baina ya kata mbili za Dung'unyi na Puma katika eneo la vijiji vya Wibia na Dung'unyi katika Mbuga ya Njori mkoani Singida.

Utatuzi wa mgogoro huo ukiendelea.


Na Mwandishi Wetu, Ikungi


MKUU wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro ameongoza kazi ya utatuzi wa mgogoro wa Ardhi baina ya kata mbili za Dung'unyi na Puma katika eneo la Vijiji vya Wibia na Dung'unyi katika Mbuga ya Njori mkoani Singida.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Mei 26, 2022 Muro alisema katika kutatua mgogoro huo alikuwa ameambatana na kamati ya usalama ya wilaya hiyo na kuwa kazi ya kwanza walioifanya baada ya kufika eneo la tukio ni kukutana na viongozi wa pande zote mbili pamoja na familia za wananchi wanaovutana katika eneo hilo hatua ambayo ilianza kuhatarisha amani na usalama wa mbuga hiyo inayotumiwa kwa kilimo na mifugo.

Wakitoa taarifa za awali Mwenyekiti wa Kijiji cha Wibia Daniel Benedict Amasi na Alex Mateo Jingu wa Kijiji cha Dung'unyi walisema mgogoro huo ulianzia katika familia mbili na kuchukua sura ya mgogoro wa vijiji kutokana na utata wa mipaka inayotengeneza vijiji vyao.

Muro alisema katika hatua ya awali ya usikilizaji wa mgogoro huo ofisi yake imeanza kusikiliza pande zote za uongozi wa vijiji, familia zinazopingana uku ikizingatia maelekezo ya mkuu wa wilaya aliyekuwepo wakati wa mapigano katika eneo hilo wakati huo ambaye sasa ni Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Miraji Mtaturu pamoja na kuziangalia hukumu za mabaraza ya ardhi zilizopo.

No comments:

Post a Comment

Pages