May 22, 2022

Huawei Tanzania yajivunia mafanikio ukuzaji ICT, utoaji ajira na ushiriki miradi mikubwa maendeleo


Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Huawei Tanzania, Tom Tao akizungumza na wadau wa kampuni mbalimbali alipokutana nao jijini Dar es Salaam.
 
 
Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

Kampuni ya Huawei Tanzania imesema katika kipindi chake cha zaidi ya miaka 13 ya uendeshaji shughuli zake nchini Tanzania imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutoa mchango mkubwa kwenye huduma ya miundombinu ya Teknolojia ya Mawasiliano (ICT) huku ikibainisha kuhudumia asilimia 75 ya Watanzania.

Aidha, kampuni hiyo katika kipindi hicho inajivunia kutengeneza ajira zaidi ya 1,000 zikiwemo za Wahandisi wa Teknolojia ya Mawasiliano pamoja na utoaji mafunzo kwa vitendo kwa wahandisi zaidi ya 2000 wa ICT.

Hayo yamesemwa jijini humo na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Huawei Nchini, Tom Tao wakati kampuni hiyo ilipokutana na wadau wa kampuni mbalimbali lengo likiwa kueleza bidhaa zao na kubadilishana mawazo.

Amesema kuwa kampuni hiyo inasaidia kutatua changamoto mbalimbali za ICT  hasahasa katika Miradi ya Kimkakati ikiwemo Mradi wa Reli ya KIsasa (SGR) hivyo inashiriki bega kwa bega na Serikali kuhakikisha mradi unakamilika kwa haraka.

Kwa upande wake, Meneja wa ICT wa Kampuni ya Redington- Tanzania, Rahul Bhati amesema ICT imesaidia kukuza uchumi ikiwemo kupunguza tatizo la ajira kwani Watanzania wanaitumia teknolojia hiyo kupashana habari na kutangaza biashara zao.

Nae, Mkurugenzi Msaidizi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Peter Mwalyasanda ameupongeza uongozi wa Huawei nchini kwa jitihada wanazozifanya za kukuza uchumi kupitia ICT.

Ameongeza kuwa Serikali imefanya marekebisho katika sheria, kanuni, sera na miongozo kwa upande wa teknolojia lengo likiwa kukuza ICT.



No comments:

Post a Comment

Pages